
Mchezaji mmoja na afisa wa timu ya taifa ya wanawake ya Iran, wameomba kupewa hifadhi na mamlaka za Australia, saa chache baada ya wenzao wengine watano kupewa hifadhi na utawala wa Canberra.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hatua yao inakuja wakati huu wanaharakati wa haki za binadamu, wakiitaka Australia kutoa hifadhi kwa wachezaji na benchi la ufundi, kufuatia hofu kuwa ikiwa watarejea nyumbani watakutana na vitendo vya unyanyasaji.
Hofu hiyo inaongezeka baada ya juma lililopita, watangazaji wa televisheni ya taifa ya Iran, kuwataja wachezaji hao kama wasaliti wa nchi baada ya kukataa kuimba wimbo wao wa taifa katika moja ya mechi ya michuano ya Asia.
Waziri wa mambo ya ndani wa Australia, Tony Burke, amesema wawili hao wanaungana na wenzao watano ambao juma hili walipewa hifadhi ya ukimbizi.
“Nilipokutana nao, niliwapa nafasi ile ile kama wenzao watano niliokutana nao usiku uliopita”, alisema Burke alipozungumza na wanahabari.
Hata hivyo kikosi kizima cha wachezaji waliosalia pamoja na benchi la Ufundi, tayari kimewasili Malaysia asubuhi huu baada ya kuondoka Sydney usiku, picha wakiwa kwenye uwanja wa Kuala Lumpur zimethibitisha.
Awali kulikuwa na hofu kuwa huenda maofisa wa timu wangewazuia wachezaji wengine na wafanyakazi kuomba hifadhi, Waziri Burke akidai kuwa wachezaji wote walitenganishwa na wenzao na kila mmoja alipewa nafasi ya kutafakari ikiwa anataka kubaki Australia au la.