Katika mkutano huu wa kila mwaka kwa wajumbe wengi vijana, si wa majadiliano pekee bali ni nafasi ya kuhakikisha wanawake hasa vijana wanashiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu za changamoto za dunia.

Mwanamke katika suti ya maroon ameketi kwenye kipaza sauti katika studio ya redio akiwa na nembo ya Umoja wa Mataifa kwenye skrini nyuma yake.

Eunice Kisiwaa Gyan, mwanaharakati kijana mwenye asili ya Ghana na anayeishi hapa Marekani.

Vijana wataka uongozi na hatua halisi

Eunice Kisiwaa Gyan, mwanaharakati kijana mwenye asili ya Ghana na anayeishi hapa Marekani, anasema vijana wanawake hawapaswi kuwa washiriki wa alama tu, bali wanahitaji kuwa sehemu ya uongozi katika masuala muhimu kama katika kila nyanja.

“Hatuko hapa kuwa kama ishara ya mfano tu. Tuko hapa kuzungumzia ushiriki wa wanawake katika amani na usalama, ushiriki wa wanawake katika hatua za tabianchi… kwa sababu bila sisi kizazi kijacho hakiwezi kuendelea kuwepo. Ndoto zenu ni muhimu, maisha yenu ni muhimu na thamani yenu ni kubwa kuliko tu sura nzuri”.”

Gyan anasema kuwa kuwapa nguvu vijana wanawake kuzungumza na kushika nafasi za uongozi ni muhimu katika kujenga jamii jumuishi zenye haki na, haki ya kisheria na hatua zaidi.

Kuongeza uelewa kuhusu mila na vitendo hatarishi

Mshiriki mwingine kijana, ni Taslimat Yusuf kutoka Nigeria, anahudhuria mkutano huo ili kuangazia changamoto zinazoendelea katika jamii yake kama ukeketaji wa wasichana na ukatili wa kijinsia. 

Anawakilisha shirika la Shirika la Sauti Moja kwa Ukombozi wa Wanawake na Watoto au One Voice Initiative for Women and Children Emancipation.

Mwanamke mweusi aliyevaa miwani na shati lenye mistari ameketi kwenye dawati la studio na kipaza sauti. Nyuma yake kuna skrini kubwa inayoonyesha nembo ya Umoja wa Mataifa. Picha hiyo imewekwa na CSW70 na SDGs.

Mshiriki wa mkutano wa CSW70 Taslimat Yusuf kutoka Nigeria.

Yusuf anasema manusura wa ukatili katika jamii yake mara nyingi huogopa kuzungumza kutokana na hofu na unyanyapaa, hivyo amesisitiza katika jukwaa hili kwamba kuna haja kubwa ya mifumo madhubuti ya msaada.

“Tunahitaji kuwapa manusura sauti na kuwajulisha kuwa hawako peke yao, wanaonekana na sauti zao zitasikika. Haki lazima itendeke kwao na hii ndio sababu niko hapa kuchagiza uelewa kuhusu ukeketaji, ukatili wa kijinsia na kuona jinsi ambavyo nitaweza kubadilishana mawazona washiriki wengine.”

Serikali zatakiwa kuunga mkono juhudi zilizopo

Taslimat pia anazitaka serikali kushirikiana na mashirika ambayo tayari yanafanya kazi ya kusaidia manusura wa vitendo hivyo badala ya kuanzisha taasisi mpya zinazoweza kurudia kazi zilizopo. Anasema kupanua wigo vituo vya msaada kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia kutasaidia waathirika kupata msaada na haki kwa haraka.

Kadri mkutano huo unavyoendelea, wanaharakati vijana wanasema ujumbe wao kwa viongozi ni wazi: ahadi lazima zibadilishwe kuwa hatua halisi ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wanawake na wasichana duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *