Dar es es Salaam. Kiongozi wa asasi za kiraia nchini Tanzania, Martina Kabisama amesema Tanzania inaendelea vizuri na mkakati wa kujijengea msingi imara wa amani, umoja na ustahimilivu wa kijamii.

Akizungumza katika mkutano Geneva nchini Uswisi, Kabisama, alitoa taarifa kuhusu maendeleo yaliyofikiwa na Tanzania katika kuimarisha haki za binadamu, mshikamano wa kijamii na majadiliano ya kitaifa, wakati wa kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva.

Kabisama, ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa mashirika ya haki za binadamu ya kusini mwa Afrika (Southern Africa Human Rights Non-Governmental – SAHRiNGON na Mkurugenzi Mtendaji wa Action for Change, alisema katika mjadala uliofanyika katika Palais des Nations kuwa Tanzania imeendelea kujijengea msingi imara wa amani, umoja na ustahimilivu wa kijamii.

Alibainisha kuwa nchi imeimarisha utawala shirikishi na ushiriki wa wananchi katika maendeleo kupitia dhamana za kikatiba zinazolinda uhuru wa kutoa maoni, kujumuika na kushiriki katika shughuli za kijamii na kitaifa. Hali hiyo imewezesha asasi za kiraia kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu ya uraia, utetezi wa sera, ufuatiliaji wa haki za binadamu na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya kidemokrasia.

Aidha, alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika haki za kijamii na kiuchumi kupitia upanuzi wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji, makazi na fursa za ajira. Kabisama pia alitaja hatua zilizochukuliwa katika kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi kupitia Sheria ya Ardhi ya Vijiji na Sheria ya Ardhi, hatua ambazo zimechangia kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za uzalishaji na kuimarisha ustawi wa kaya.

Kwa upande wa vijana, alisisitiza umuhimu wa uwekezaji katika elimu, ujuzi, ubunifu na teknolojia kama msingi wa kujenga taifa lenye maendeleo jumuishi na endelevu. Hata hivyo, alitaja changamoto zinazohitaji juhudi za pamoja, ikiwemo tofauti za maendeleo kati ya maeneo na upatikanaji usio sawa wa baadhi ya huduma za msingi.

Kabisama alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, pamoja na kudumisha dhamira ya kisiasa katika kusukuma mbele ajenda ya haki za binadamu na maendeleo jumuishi. Aliongeza kuwa ushirikiano kati ya asasi za kiraia na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni muhimu katika kukuza uwajibikaji, upatikanaji wa haki na kulinda maslahi ya makundi yaliyo hatarini.

Aliutaja mchango wa asasi za kiraia katika elimu ya uraia, msaada wa kisheria na ufuatiliaji wa haki za binadamu, akieleza kuwa umeendelea kusaidia wananchi kutambua haki zao na kushiriki kikamilifu katika maendeleo. Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ilitajwa kama hatua muhimu ya kupanua wigo wa huduma za haki kwa wanawake, watoto na makundi mengine yenye uhitaji.

Katika hitimisho, Kabisama alisisitiza kuwa heshima kwa utu wa binadamu inapaswa kuwa msingi wa maendeleo endelevu, amani ya kijamii na mshikamano wa taifa. Aliweka mfano wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan unaojengwa kwenye misingi ya 4Rs: Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Ujenzi Upya, unaotoa nafasi kwa Tanzania kuimarisha utawala bora, mshikamano wa kitaifa na mageuzi yanayowagusa wananchi.

Ushiriki wa Kabisama katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaonyesha nafasi inayozidi kuimarika ya asasi za kiraia za Tanzania katika majukwaa ya kimataifa na dhamira ya nchi kuendeleza haki za binadamu, majadiliano ya kitaifa na maendeleo jumuishi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *