
Dar es Salaam. Kongamano la Uwekezaji Afrika Mashariki la mwaka 2026 (East Africa Investment Forum – EAIF 2026) linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kutoa fursa kwa vijana wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia, huku wadau wakijadili sera na mikakati ya kukuza uchumi wa kidijitali katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kongamano hilo litakalofanyika Dar es Salaam Machi 26 na 27, 2026, linatarajiwa kukutanisha wadau wa sekta ya teknolojia ya fedha (fintech), wawekezaji, watunga sera, wabunifu wa teknolojia na wajasiriamali ili kujadili namna ya kuharakisha ukuaji wa sekta ya kidijitali na kuongeza uwekezaji katika ukanda huo.
Akizungumza Dar es Salaam leo Ijumaa Machi 13, 2026 wakati wa kuitambulisha kampuni ya Vodacom Tanzania na huduma ya M-Pesa kama wadau wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Chama cha Watoa Huduma za Kifedha kwa Kutumia Teknolojia (Tafina), Shadrack Kamenya, amesema kongamano hilo litakuwa jukwaa muhimu la majadiliano kuhusu sera na mazingira ya uwekezaji katika sekta ya fintech.
“EAIF 2026 inalenga kuwakutanisha wadau mbalimbali ili kujadili sera na mikakati itakayowezesha ukuaji wa fintech na kuvutia uwekezaji zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki,” amesema Kamenya.
Mwakilishi wa Vodacom Tanzania, Buberwa Mukurasi, amesema ushiriki wa kampuni hiyo katika kongamano hilo unalenga kutoa nafasi kwa vijana kujifunza, kubadilishana mawazo na kujenga ushirikiano na wawekezaji pamoja na wadau wa sekta ya teknolojia.
“Tunaamini vijana wana nafasi kubwa katika mapinduzi ya uchumi wa kidijitali. Kupitia kongamano hili watapata fursa ya kuonesha ubunifu wao, kujifunza kutoka kwa wataalamu wa sekta na kujenga mitandao itakayowasaidia kukuza biashara zao,” amesema Mukurasi.
Kupitia majadiliano hayo, washiriki wanatarajiwa kubaini fursa mpya za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na Serikali pamoja na kuweka mikakati itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi.
Aidha, kongamano hilo linatarajiwa kuwa jukwaa la kuibua mawazo mapya ya kiteknolojia yatakayosaidia vijana kujiajiri, kukuza biashara za kidijitali na kuchochea ajira katika uchumi unaoendelea kubadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia.
Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za robo ya mwaka 2025 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hadi kufikia Septemba 2025 kampuni ya Vodacom ilikuwa na asilimia 31.5 ya soko la mawasiliano ya simu nchini.
Naye Meneja wa Mahusiano wa Tafina, Juliet Kiluwa, amesema kongamano hilo litahusisha mijadala ya kitaalamu, mikutano ya kuunganisha wadau wa biashara na majadiliano ya kimkakati kuhusu ukuaji wa sekta ya fintech.
Amesema pia kongamano hilo litasaidia kuunganisha miradi ya maendeleo na fursa za ufadhili kupitia teknolojia, ubunifu na ushirikiano wa kisekta.
Kwa sasa, Tafina ina wanachama zaidi ya 80 wanaounda jumuiya ya watoa huduma za kifedha kwa kutumia teknolojia nchini.