
Waziri Mkuu wa Japan amesema wazi katika kikao cha bunge kwamba nchi yakehaina mpango wa kutuma vikosi vya kijeshi kwa ajili ya operesheni za kuondoa mabomu ya baharini katika Lango Bahari la Hormuz.
Kwa mujibu wa Pars Today, Sanae Takaichi akijibu maswali ya wabunge wa Japan, amekanusha taarifa zilizodai uwezekano wa nchi hiyo kushiriki katika operesheni za kijeshi za uhandisi katika Lango Bahari la Hormuz. Ameongeza kuwa licha ya ripoti zinazoleta wasiwasi kuhusu madai ya kuwepo kwa mabomu ya baharini katika maji ya njia hiyo muhimu ya baharini, Japan inatafuta suluhisho za kidiplomasia na zisizo za kijeshi ili kulinda usalama wake wa nishati.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasimamia kikamilifu Lango Bahari la Hormuz—moja ya njia muhimu zaidi za usafiri wa majini duniani—kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Hakuna meli inayopita hapo bila idhini ya Iran hivi sasa.
Wakati huo huo, matokeo ya kura mpya ya maoni iliyofanywa na shirika la habari la Japan, Jiji Press, yanaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wa Japan wanapinga mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran. Wataalamu wa sheria za kimataifa pia wamesisitiza kuwa uvamizi wa kijeshi wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa. Uvamizi huo sasa umeibua matatizo makubwa ya kiuchumi duniani na kuathiri maisha ya mabilioni ya watu.