
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon ametangaza kuwa, harakati hiyo imejiandaa kwa ajili ya mapambano ya muda mrefu.
Sheikh Naim Qassim alisema jana usiku katika hotuba yake kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Quds kwamba kukaliwa kwa mabavu Palestina ni ukandamizaji mkubwa sana katika historia ya wananchi wa Palestina na kwamba siku ya Kimataifa ya Quds ni nembo na ina nafasi muhimu katika kutoa wito wa kukombolewa Palestina na pia katika kueneza ujumbe huo kwa watu wote wanaodhulumiwa duniani ili kujiondoa katika mnyonyoro wa utumwa na ukandamizaji.
Katibu Mkuu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon amesema: Uvamizi unaofanywa na adui Mzayuni na Marekani dhidi ya kanda hii na duniani kwa ujumla ni matokeo ya kupandikizwa donda la saratani ambalo kwa zaidi ya miaka 70 halijaruhusu kupatikana amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia.
Mwishoni mwa hotuba yake Sheikh Naim Qassim ameeleza kuwa wanamuqawama wa Hizbullah wanapenda kufa shahidi, hawaogopi kufa na wako tayari kukabiliana moja kwa moja na adui. Amesisitiza kuwa: “Tumeajiandaa kwa mapambano ya muda mrefu na adui Mzayuni na Marekani watachanganyikiwa katika medani ya vita.”