TANGA: MKUU wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, Salum Nyamwese, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kudumisha mshikamano na utamaduni wa kusaidiana, huku akiongoza harambee maalum ya kuchangia makundi yenye uhitaji kuelekea sikukuu ya Eid al-Fitr.
Katika hafla hiyo ya Iftar iliyoandaliwa na ofisi yake na kuwakutanisha viongozi wa dini, serikali na wananchi, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian, ameunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia Sh milioni 1 kusaidia wenye mahitaji.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, DC Nyamwese alisema lengo la kukutana na kufuturu pamoja ni kuimarisha uhusiano kati ya viongozi na wananchi, sambamba na kuwakumbusha wenye nacho wajibu wao wa kuwajali wasiojiweza.
”Mshikamano na umoja wetu ndio msingi mkuu wa amani na maendeleo tuliyonayo Handeni. Ni muhimu kila mmoja akaguswa kusaidia makundi maalum kama yatima, wazee na watu wenye ulemavu ili kuimarisha ustawi wa jamii yetu,” alisema DC Nyamwese.
Mapema kabla ya kuanza kwa hafla hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya alitembelea Gereza la Wilaya ya Handeni ambapo alitoa msaada wa bidhaa mbalimbali kwa wafungwa na mahabusu.
Alibainisha kuwa hatua hiyo ni sehemu ya kuonyesha upendo na kuwafanya wahusika wajione kuwa ni sehemu ya jamii, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea kilele cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na sikukuu ya Eid.
Viongozi wa dini waliohudhuria hafla hiyo walipongeza hatua ya DC Nyamwese kwa kuunganisha jamii na kusema kuwa vitendo hivyo vya huruma ni fundisho tosha la imani na utu.