Sarkozy, mwenye umri wa miaka 70, alihukumiwa Alhamisi kwa kosa la kupanga njama ya kupata ufadhili haramu kutoka kwa kiongozi wa Libya wa wakati huo, Muammar Ghadhafi, kwa ajili ya kampeni yake ya urais mwaka 2007. Ni mara yake ya tatu kukutwa na hatia, lakini sasa hatoweza kuepuka jela licha ya kuahidi kukata rufaa.
Baada ya uamuzi huo, Sarkozy alisema ataheshimu wito wa mahakama na, akisisitiza kuwa hana hatia, alionya: “Kama wanataka nikalale jela, nitalala, lakini nikiwa nimeinua kichwa changu juu.”
Sarkozy ambaye amaezaliwa Januari 28, 1955, ni mwana wa mkimbizi kutoka Hungary. Akiwa na shahada ya sheria, aliingia siasa akiwa na mtindo tofauti na viongozi wengi wa Kifaransa waliopitia shule ya kifahari ya ENA. Alishinda urais mwaka 2007 akiwa na umri wa miaka 52, akiahidi kuleta nguvu mpya na msimamo mkali kuhusu uhamiaji, usalama na utambulisho wa kitaifa.
Sarkozy alianza kwa kishindo kwenye majukwaa ya kimataifa, lakini urais wake ulitikiswa na mdororo wa kifedha wa mwaka 2008. Aliondoka madarakani mwaka 2012 akiwa na viwango vya chini zaidi vya umaarufu kwa rais wa Ufaransa tangu vita vya pili vya dunia. Tukio la kumbukumbu ni pale alipomtupia matusi mkulima kwenye maonyesho ya kilimo mwaka 2008, jambo lililomchafua zaidi kisiasa.
Kuteleza kisiasa
Sarkozy alishindwa tena na François Hollande katika uchaguzi wa 2012, akawa rais wa kwanza tangu Valery Giscard d’Estaing kunyimwa muhula wa pili. Aliahidi wakati huo: “Hamtanisikia tena.” Lakini badala yake alirejea kwenye ulingo wa siasa, akashindwa tena kuwania urais kupitia chama chake mwaka 2017.
Licha ya matatizo yake ya kisheria, Sarkozy aliendelea kuvutia macho ya umma kwa ndoa yake na mwanamuziki na mwanamitindo maarufu Carla Bruni. Alibaki kuwa mshawishi wa ndani kwenye siasa za mrengo wa kulia, huku akikutana mara kwa mara na Rais Emmanuel Macron.
Sarkozy sasa anabeba rekodi mbaya miongoni mwa marais wa Ufaransa wa kisasa. Wakati mtangulizi wake Jacques Chirac pia alihukumiwa kwa ufisadi, Sarkozy ndiye rais wa kwanza wa baada ya vita ya pili ya dunia kuhukumiwa mara mbili na kupewa adhabu ya kifungo cha moja kwa moja. Tayari amevuliwa heshima ya juu kabisa ya taifa, Legion d’Honneur.
Kwa hukumu hii, Sarkozy anakuwa kiongozi wa kwanza wa Ufaransa kwenda jela tangu Philippe Petain, aliyekuwa kiongozi wakati wa utawala wa Ujerumani wa Kinazi.
Kwa wengi, hili ni somo la kisiasa kwamba hata viongozi waliopata heshima kubwa wanaweza kukumbwa na anguko kubwa kutokana na kashfa za ufisadi.