Waumini wa dini ya Kiislamu Mkoa wa Morogoro wamepongezwa kwa kuendelea kudumisha utulivu, umoja na mshikamano licha ya nchi kupitia changamoto za kisiasa zilizoambatana na matukio ya uvunjifu wa amani yaliyoripotiwa Oktoba 29 katika baadhi ya maeneo nchini. Hali ya utulivu iliyopo mkoani humo imetajwa kuwa matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya wananchi, viongozi wa dini na Serikali katika kulinda amani ya Taifa.
Akitoa salamu za Serikali katika hafla ya Iftar iliyowakutanisha waumini pamoja na viongozi wa dini na Serikali, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala amesema wananchi wa Morogoro wanapaswa kuendelea kuwa walinzi wa kwanza wa amani kwa kuimarisha mshikamano, uvumilivu na kuheshimiana katika jamii.
Amesema utulivu wa Mkoa wa Morogoro ni mfano mzuri kwa maeneo mengine nchini, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuitunza na kuilinda.
Kwa upande wake, Mwanazuoni na Mhadhiri wa Kimataifa wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Rashid Mziwanda amesema ni muhimu kwa viongozi wa dini kutumia majukwaa yao kuhubiri amani, upendo na mshikamano ili kuimarisha utulivu wa Taifa.
Aidha, Sheikh Mziwanda ametoa onyo kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaojihusisha na matamko yanayoweza kuiingiza nchi katika hali ya taharuki, akiwataka kutanguliza busara na kutumia nafasi zao kuunganisha jamii badala ya kuibua migawanyiko.
(Feed generated with FetchRSS)