Mpango wa Serikali wa kupanga na kusimamia matumizi bora ya ardhi, unaoratibiwa na Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, umetajwa kuwa njia muhimu ya kumaliza migogoro ya ardhi katika jamii pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
Akizungumza katika Kijiji cha Tawa Tarafa ya Matombo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, mara baada ya kikao na wananchi wa kijiji hicho, Afisa Ardhi Mwandamizi kutoka Tume ya Taifa ya Mipango ya Matumizi ya Ardhi, Mkwaya Songo, amesema kuwa mpango wa kupanga matumizi bora ya ardhi utasaidia kuondoa mwingiliano wa matumizi ya ardhi katita shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji na Vijijini kutoka Tume hiyo, Philemon Moi, amesema kuwa utekelezaji wa mpango huo umefika katika wakati muafaka kwani utawawezesha wananchi kupanga na kutumia maeneo yao kwa utaratibu unaoeleweka.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Tawa, Wilfred Kunambi, amesema kuwa utekelezaji wa mpango huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza changamoto za migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwasumbua baadhi ya wananchi.
Baadhi ya wananchi, akiwemo George Msumi na Salome Malick, wameipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango unaolenga kuhakikisha kila Mtanzania anaishi kwa amani, furaha na utulivu, huku wakifanya shughuli zao za kila siku bila kukumbana na changamoto zisizo za lazima.
(Feed generated with FetchRSS)