MTWARA: WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kupitia Kanda ya Kusini imezalisha miche zaidi ya 2,000,000 na kugawa kwa jamii, taasisi za umma, Shule za msingi na sekondari na sekta binafsi wakiwemo na wawekezaji viwanda wanajihusisha na biashara za mbao katika ukanda huo.
Mhifadhi Misitu wa Wakala huo kutoka kitengo cha ugani na uenezi wa Kanda ya Kusini , Lightness Chale amesema hayo katika Shule ya Sekondari Shangani, kata ya Shangani Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara- Mikindani Wilaya ya Mtwara.
Chale amesema kuwa uzalishaji wa miche ulifikia 2,018,000 kutoka kwenye vitalu 10 na kufikisha lengo la uzalishaji uliowekwa wa miche 2,000,000 mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema pamoja na kufikia lengo la uzalishaji huo, wakala umeweza kugawa bure miche milioni 1,416,000 katika taasisi za umma, shule za msingi na sekondari, sekta binafsi na wananchi kwenye ukanda wa kusini unaojumuisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

Chale amesema miche iliyozalishwa kwa wingi ni ya mbao ikiwemo ya asili ya aina mbalimbali kama mkongo,Mninga na mivule na hiyo ni kutokana na uhitaji wa wateja ambao wanajihusisha na biashara za mbao katika ukanda wa kusini
“Tumezalisha miche mingi ya mbao ili ipandwe ukanda huu kwa ajili ya kupunguza ule uhitaji na kuwawezesha wavune kwa sasa na baadaye,”amesema Chale.
Chale amesema uzalishaji mengine ni wa miche ya matunda ikiwemo ya mipera, michungwa, papai na parachichi,na unalenga jamii iwaweze kuipanda ili kupata madunda ambayo watayatumia kama chakula na biashara kwa lengo la kujipatia vipato na kukuza uchumi wao.
“Hivyo TFS Kanda ya Kusini inatoa rai kwa wananchi wote kufika kwenye ofisi zao za wilaya na kuichukua miche hiyo kwani miche ingali ya kutosha waweze kupanda maeneo yao na kurudishia kwenye hifadhi za vijiji,”amesema Chale.
“TFS inaigawa miche ya miti kwa jamii bure, na kumekuwa na mwitikio mkubwa kwa makundi yote kuanzia jamii, taasisi za umma za ukanda huu tangu mvua zilipoanza , miche imechukuliwa kwa wingi,”amesema Chale.
Kwa Upande wake Kaimu Mhifadhi Wilaya ya Mtwara, Ashraf Hussein amesema katika wilaya hiyo ina misitu ya hifadhi mitatu ambao ni Ziwani, Naliendele na misitu ya hifadhi ya mikoko.
Ashraf amesema kumekuwa na programu za utoaji elimu kwa wananchi juu ya upandaji wa miti na uhifadhi wa misitu kwa ujumla na ugawaji wa miche ya miti bure kila mwaka kwa wananchi wanaiomba kwenda kupata maeneo yao.
“ Ipo hamasa kubwa kwa vikundi hasa vya wanawake upandaji miti na utunzaji misitu, ndivyo vinavyozalisha asali nyingi kutokana na mikoko iliyohifadhiwa na wanawake,” amesema Ashraf.
Kila mwaka Machi 21 ni Siku ya Misitu Duniani na siku ya upandaji miti kitaifa ambapo kwa mwaka huu Kitaifa itafanyika mkoani Lindi.