Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amewataka madereva kuwa mabalozi wa usalama barabarani kwa kuifikisha elimu waliyoipata kwa madereva wenzao na jamii kwa ujumla, hatua itakayosaidia kupunguza ajali na kuimarisha utamaduni wa kuzingatia sheria za barabarani.
Itunda ameyasema hayo katika ufunguzi wa mafunzo ya kuwajengea uwezo madereva wakiwemo askari na watumishi wa taasisi mbalimbali za umma katika Mkoa wa Mbeya alipokuwa amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Itunda amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha usalama barabarani, ikiwemo kuwajengea uwezo madereva wanaoendesha vyombo vya moto katika taasisi za umma ili kupunguza ajali zinazoweza kuepukika.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuongeza uelewa kwa madereva kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani pamoja na kuendesha vyombo vya moto kwa uangalifu na nidhamu.
Itunda amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha wanatumia ipasavyo elimu watakayoipata ili kuongeza ufanisi katika kazi zao na kuchangia kulinda maisha ya watumiaji wa barabara pamoja na mali.
Zaidi ya askari na watumishi wa umma 180 kutoka taasisi mbalimbali katika Mkoa wa Mbeya wanashiriki katika mafunzo hayo, ambayo yanatarajiwa kuimarisha nidhamu na ufanisi katika uendeshaji wa vyombo vya moto na kuchangia juhudi za Serikali za kupunguza ajali barabarani.