Mbeya. Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda, amewahimiza viongozi wa dini ya Kiislamu kuendelea kusimamia na kuimarisha maadili kwa waumini katika kipindi chote cha maisha, hata baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ili kulinda amani na utulivu ambao ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
Itunda ametoa wito huo leo wakati wa hafla ya Iftari iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella. Hafla hiyo imelenga kuimarisha mshikamano, upendo na ushirikiano miongoni mwa waumini wa Kiislamu, watumishi wa Halmashauri, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi wa Wilaya ya Mbeya.
Akizungumza katika hafla hiyo, Itunda ameeleza kuwa Ramadhan ni mwezi mtukufu sana kwa Waislamu, unaobeba mafunzo muhimu ya kiroho na kijamii. Amesema ni kipindi cha ibada, toba, subira, huruma na kujitafakari, ambapo waumini hufunga kwa ajili ya kumtii Mwenyezi Mungu na kuimarisha ucha Mungu wao kama ilivyoelekezwa katika Qur’an tukufu.
Ameongeza kuwa maadili yanayojengwa wakati wa Ramadhan yanapaswa kuendelea kudumishwa katika maisha ya kila siku hata baada ya mwezi huo kumalizika.
“Niwaombe sana viongozi wa dini kuendelea kuhamasisha waumini kutenda mema hata baada ya Ramadhan kupita. Kama viongozi wa umma, tunalo jukumu la kuendeleza maadili ya uadilifu, upendo, huruma na kuwahudumia wananchi kwa haki,” amesema Mhe. Itunda.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu, akieleza kuwa hayo ni nguzo muhimu katika kufanikisha juhudi za maendeleo. Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na upanuzi wa barabara kutoka Igawilo hadi Tunduma, ambayo inalenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na biashara. Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unahitaji mazingira ya amani na mshikamano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Hafla hiyo ya Iftari iliyoandaliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Erica Yegella, imefanyika kwa mara ya pili mfululizo tangu aingie madarakani, ambapo imewakutanisha watumishi wa Halmashauri wakiwemo wakuu wa idara, maafisa mbalimbali, wadau wa maendeleo ya wilaya, wafanyabiashara, viongozi wa dini pamoja na wananchi, ikiwa ni sehemu ya kujenga mshikamano na kuimarisha ushirikiano katika kuleta maendeleo ya Wilaya ya Mbeya.