Katika ujumbe wake, Katibu Mkuu amebainisha kuwa waislamu bilioni 2 duniani wanatoka katika maeneo mbalimbali ya dunia na kuakisi utofauti wa ubinadamu.

Ubaguzi dhidi ya uislamu

Hata hivyo, amesema kuwa bado mara nyingi hukabiliwa na ubaguzi, kutengwa kiuchumi na kijamii, sera za uhamiaji za kibaguzi, pamoja na ufuatiliaji na uchambuzi wa wasifu wao bila msingi.

Ameonya kuwa mienendo hiyo ni ya kutia hofu na mara nyingi huchochewa na chuki dhidi ya Uislamu, hali inayoweza kusababisha unyanyasaji na hata ukatili dhidi ya watu binafsi na maeneo ya ibada.

Hatua za serikali

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa serikali zinapaswa kuchukua hatua thabiti dhidi ya kauli za chuki, kulinda uhuru wa kuabudu, na kupambana na aina zote za ubaguzi kwa kuhakikisha uzingatiaji kamili wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.

Aidha, ametoa wito kwa majukwaa ya mtandaoni kushirikiana katika kutokomeza kauli za chuki na unyanyasaji dhidi ya watu kwa misingi ya dini au imani zao.

Pia Guterres amehimiza watu wote kupaza sauti kupinga chuki, chuki dhidi ya wageni, na ubaguzi popote vinapotokea.

Uteuzi wa Mjumbe Maalum

Amekumbusha  kuwa mwezi Mei 2025 alimteua Mwakilishi wa Ngazi ya Juu wa Ushirikiano wa Ustaarabu kuwa Mjumbe Maalum wa  Umoja wa Mataifa wa kutokomeza chuki dhidi ya uislamu, ili kuimarisha juhudi za pamoja za kupambana na tatizo hilo.

Akihitimisha ujumbe wake, Katibu Mkuu ametoa wito wa kurejea katika ahadi ya usawa, haki za binadamu na utu kwa kila mtu bila kujali imani yake. Guterres amesisistiza kuwa chuki dhidi ya uislamu inapaswa kutokomezwa kabisa katika kila nchi na jamii duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *