GEITA: MWENYEKITIi wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,  Subira Mgalu, amesema serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kusambaza umeme ili kuhakikisha wananchi wanaoishi pembezoni mwa miji na vijiji wanapata huduma hiyo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Akizungumzia mafanikio ya miradi ya kusambaza umeme Machi 15, 2026 katika kitongoji cha Elimu Kijiji cha Mshinde mkoani Geita, Magalu amesema kuwa Miradi inayotekelezwa inalenga kupanua wigo wa huduma ya umeme katika vitongoji 15 kwa kila jimbo la uchaguzi HEP 2(A) pamoja na mradi mkubwa wa kusambaza umeme kwenye vitongoji 9,009 Tanzania nzima Geita ikiwemo.

Pia Mwenyekiti huyo ameigaza Kampuni ya CCC Beijing Industrial & Commercial Co. Ltd, ambayo inatekeleza miradi mingi mkoani Geita kuhakikisha hadi kufikia Machi 28, 2026 inakamilisha mrradi ambapo kwa sasa utekelezaji wake ulikuwa umefikia asilimia 80 kukamilika haraka.

Kwa upande wake Naibu Waziri, Wizara ya Nishati,  Salome Makamba amewapongeza Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kuendelea kuisimamia vyema sekta ya nishati pamoja na ukaribu wao katika kufuatilia miradi ya kusambaza nishati ya umeme hadi kwenye vitongoji.

“Kipekee naipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kufika hadi kwenye vitongoji kuangalia utelekezaji wa miradi ya kimaendeleo; ikiwemo hii ya kufikisha umeme kwenye kitongoji cha elimu hapa katika kijiji cha Mshinde, hii ni mara ya kwanza kwa ugeni kama huu kufika mahali hapa,” amesema Makamba

Katika taarifa yake ya awali; Mkurugenzi wa Umeme Vijijini, Mhandisi, Jones Olotu ambaye pia alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA alisema Mkoa wa Geita una jumla ya vijiji 486 na vitongoji 2,195, kupitia Miradi mbalimbali tayari huduma ya umeme imefika katika vijiji vyote 486 pamoja na vitongoji 1,193.

Mhandisi Olotu aliongeza kuwa ipo miradi kadhaa ya kusambaza umeme kwenye vitongoji inayoendelea katika Mkoa wa Geita ambapo baada ya kukamilika, mkoa huo utakuwa na jumla ya vitongoji 1,895 ambavyo vitakuwa na huduma ya umeme na kubakia vitongoji 300 tu ambavyo vitapatiwa huduma hiyo, ifikapo mwaka 2030.

Mhandisi, Olotu amesema serikali itaendelea kuhakikisha wananchi wengi wa mkoa huo wanafikiwa na huduma ya umeme ili kuchochea maendeleo na kuboresha maisha yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *