Wanadiplomasia nchini Pakistan wamedai mashambulizi ya nchi hiyo dhidi ya Afghanistan ndio chanzo cha kuibuka kwa matukio ya ugaidi nchini humo na kusababisha upotevu wa mali na vifo.

Wakizungumza wakati wakihojiwa na mtandao wa Dawn, wamesema kama nchi hiyo ina ulazima wa kuishambulia Afghanistan, inapaswa kuimarisha usalama wake kwanza.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo mbalimbali vya habari nchini Pakistan, watu 36 waliuawa katika tukio la bomu la kujitoa mhanga Februari 6 mwaka huu, 170 kujeruhiwa huku  tukio la ugaidi eneo la Bajaur lilisababisha vifo vya askari 11.

‘’Kama ni lazima kuishambulia Afghanistan basi usalama unapaswa kuimarishwa kwa kiasi kikubwa…, haina maana nchi inasema inapambana na ugaidi nje ya mipaka  wakati ndani ya nchi husika wananchi wake wanauawa katika matukio ya ugaidi,’’ alidai Syed Khan.

Maoni hayo ya wananchi yamekuja ikiwa zimepita siku chache tangu Pakistan kufanya mashambulizi katika majimbo ya Afghanistan ya Nangarhar, Paktika na Khost, ikidai kulenga makundi mbalimbali ya ugaidi.

Hata hivyo, mamlaka nchini Afghanistan zilibainisha kuwa mashambulizi hayo yalilenga makazi ya watu na kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo vya watu 18

‘’Huu haukuwa uharibifu wa bahati mbaya bali matokeo yanayotabirika ya Pakistan kuchagua kushambulia nchi yenye uwezo mdogo wa ulinzi wa anga, ikijua kwamba kuwa kufanya hivyo ni kuhatarisha usalama wa raia wake,’’ alisema mwananchi mwingine, Hussein Rahbi.

Baada ya vikosi vya Pakistan kushambulia Kabul na majimbo mengine ya Afghanistan, naibu msemaji wa serikali ya Afghanistan, Hamdullah Fitrat aliishutumu Pakistan kwa kulenga makazi ya raia , akibainisha kwamba wengi wa waliouawa walikuwa wanawake na watoto.

Hali hiyo iliwaibua wachambuzi wa masuala ya ulinzi na usalama Pakistan na kukosoa mashambulizi hayo wakibainisha kuwa usalama ulipaswa kuimarishwa ndani ya nchi kwanza huku serikali ya nchi hiyo ikisisitiza mpango wake wa kukabiliana na makundi ya ugaidi ndnai na nje ya nchi hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *