Dar es Salaam. Wanaume wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kuwasaidia wanawake wakati wa ujauzito na kujifungua ili kulinda maisha ya mama na mtoto na kuimarisha ustawi wa familia.

Wito huo umetolewa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utepe Mweupe yaliyofanyika Machi 15, 2026, siku inayoadhimishwa kila mwaka duniani kuwakumbuka wanawake waliopoteza maisha kutokana na matatizo ya ujauzito, uchungu au kujifungua.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mratibu wa Kitaifa wa Huduma za Uzazi Salama kutoka Wizara ya Afya, Dk Phineas Sospeter, amesema ujauzito ni safari ndefu yenye changamoto nyingi, hivyo ushiriki wa wanaume katika hatua zote ni muhimu ili kuhakikisha mama anapata huduma bora za afya.

Amesema wanaume wanapaswa kuwa karibu na wake zao katika kipindi chote cha ujauzito kwa kuwasaidia mahitaji ya msingi, kuwapa faraja na kuwahamasisha kuhudhuria kliniki mapema na mara kwa mara.

“Ujauzito ni safari ndefu na haimaliziki hadi mama ajifungue salama na mtoto awe salama. Hivyo kila mmoja, hususani mwanaume, ana wajibu wa kuhakikisha mama anapata huduma stahiki,” amesema Dk Sospeter.

Ameongeza kuwa heshima kwa mama inaonekana kupitia vitendo, ikiwemo kumsaidia majukumu ya nyumbani na kuhakikisha anapata huduma za afya kwa wakati.

Aidha, amesema huduma za afya ya uzazi ni alama ya matumaini katika jamii kwa kuwa zinaonyesha dhamira ya kulinda uhai wa mama na mtoto. Alisema juhudi zinaendelea kufanywa kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wanawake wengi zaidi, hususan wanaoishi maeneo ya pembezoni.

“Huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na wataalamu wa afya ili kuwasaidia wanawake wajawazito kupata huduma bora kuanzia wanapopata ujauzito hadi wanapojifungua,” amesema.

Washiriki wa maadhimisho ya siku ya utepe duniani wakiwakumbuka wanawake waliopoteza maisha kutokana na uzazi , maadhimisho hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).

Kwa upande wake, mkunga kutoka Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Lucy Mabada, amesema kuna uhitaji mkubwa wa kuongeza idadi ya wakunga ili kuboresha huduma za afya ya uzazi na kupunguza changamoto zinazoweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto.

Amesema wakunga ndiyo wanaokaa karibu zaidi na mama mjamzito kwa kumhudumia wakati wa ujauzito, kujifungua na baada ya kujifungua.

“Kwa kweli sisi wakunga tunakuwa karibu sana na mama mjamzito katika hatua zote za uzazi. Ndiyo maana tunaona umuhimu wa kuongeza wakunga zaidi ili kuboresha huduma hizi,” amesema Mabada.

Ameongeza kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha dunia inahitaji kuongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya wakunga ili kuboresha huduma za uzazi na kuokoa maisha ya mama na watoto wachanga.

Naye mjumbe wa bodi ya Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania, Prudence Masako, amewahimiza wazazi kushiriki kikamilifu katika huduma na programu za afya ya mama na mtoto ili kusaidia kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa ujauzito na malezi ya watoto.

“Tunafurahi kuona wazazi wengi wakifika katika programu hizi wakiwa na watoto wao. Hii inaonyesha mwitikio mzuri wa jamii katika kujifunza masuala ya afya ya mama na mtoto,” amesema Masako.

Kwa upande wake, mzazi Leah Simon amesema alipata msaada mkubwa kutoka kwa wahudumu wa afya baada ya kukumbana na changamoto wakati wa kujifungua.

Amesema awali alipata uchungu mdogo wa kujifungua na baada ya kufika hospitali aliambiwa bado haujafikia kiwango cha kujifungua hivyo aliruhusiwa kurejea nyumbani.

“Baadaye nilipata tatizo la kutokwa na damu kabla ya uchungu kuanza vizuri, lakini wahudumu wa Kituo cha Afya Kigamboni walinisaidia na hatimaye nikajifungua salama,” amesema.

Amesema huduma na uangalizi alioupata uliokoa maisha yake na ya mtoto wake, huku wahudumu wa afya wakiendelea kumfuatilia hata baada ya kujifungua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *