Viongoni wa dunia wataka vita kukomeshwa SudanViongoni wa dunia wataka vita kukomeshwa Sudan

Mkurugenzi wa mradi wa kimataifa unaoshughulikia migogoro katika eneo la Upembe wa Afrika, Alan Boswell, amesema mkutano wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka huu, unaokamilika Jumatatu, unaweza kuwa “wa kuamua” iwapo vita Sudan vitakomeshwa.

Katika taarifa yake alisema: “Kwa mara ya kwanza tangu vita vilipoanza zaidi ya miaka miwili iliyopita, nguvu kuu za kigeni zenye ushawishi mkubwa kwa Sudan zimekubaliana mwezi huu juu ya njia ya kumaliza vita,” jambo linaloleta jukumu kubwa la kushawishi pande zinazopigana Sudan kukomesha mapigano.

Sudan ilitumbukia vitani katikati ya Aprili 2023, wakati mvutano wa muda mrefu kati ya makamanda wa jeshi na wanamgambo ulipozuka katika mji mkuu Khartoum, kisha ukaenea Darfur Magharibi na sehemu nyingi za nchi hiyo.

Katika hatua muhimu baada ya msururu wa mazungumzo, Marekani, Saudi Arabia,Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu walitoa taarifa ya pamoja Septemba 12, wakitoa wito wa kuwepo usitishaji wa mapigano kwa miezi mitatu ya mwanzo ili kuruhusu misaada muhimu kufikishwa kote Sudan, ikifuatiwa na usitishaji mapigano wa kudumu.

Baada ya hapo, nchi hizo nne zinapendekeza mchakato jumuishi na wa uwazi wa mpito uzinduliwe na kukamilishwa ndani ya miezi tisa ili kutimiza matarajio ya wananchi wa Sudan ya kuanzisha serikali huru inayoongozwa na raia, yenye uhalali mpana na uwajibikaji.

Kundi hilo, linalojiita Quad, lilikutana Jumatano pembezoni mwa mkutano huo kujadili utekelezaji wa mpango huo. Mkutano mwingine wa kujadili namna ya kupunguza vita pia ulifanyika Jumatano kati ya Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na mawaziri wa mambo ya nje wa Ujerumani, Ufaransa na Uingereza. Wawakilishi wa Quad, nchi zingine zaidi ya kumi na mbili, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, Umoja wa Mataifa na kikundi cha kikanda cha Afrika Mashariki (IGAD) pia walihudhuria.

RSF yashutumiwa kwa kwa “mauaji ya kimfumo na mateso

Sudan | Wanamgambo wa RSF- wanaoongozwa na Jenarali Mohammed Dagalo
Wanamgambo wa RSF washutumiwa kwa “mauaji ya kimfumo na matesoPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Taarifa iliyotolewa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uingereza, Denmark, Norway na Kanada baada ya mkutano huo ilizihimiza serikali inayopigana na wanamgambo wa kundi la (RSF) kuanza tena mazungumzo ya moja kwa moja ili kufikia usitishaji wa mapigano wa kudumu.

Taarifa hiyo ilikaribisha tamko la Septemba 12 la Quad, na kuonyesha kuunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya “za kuratibu juhudi za kimataifa na za pande mbili za kushinikiza pande zote za Sudan kuelekea usitishaji mapigano, hatua za kibinadamu na mazungumzo ya kisiasa.” Taarifa hiyo pia ililaani vikali ushiriki wa kijeshi wa nchi za kigeni ambazo hazikutajwa majina pamoja na “vikundi visivyo vya kiserikali” na kuwataka waache kuchochea vita hivyo.

Akihutubia mkutano huo siku ya Alhamisi, Waziri Mkuu wa serikali ya Mpito ya Sudan, Kamil El-Tayeb Idris, aliishutumu RSF kwa “mauaji ya kimfumo na mateso, uporaji, ubakaji, udhalilishaji na uharibifu wa kinyama wa kila kipengele cha maisha,” kama sehemu ya juhudi zake “za kutaka kuidhibiti Sudan, kupora utajiri wake na kubadilisha muundo wa idadi ya watu wake.”

“Jumuiya ya kimataifa – na ninyi ndiyo viongozi wa jumuiya ya kimataifa – lazima mfanye kazi ya kusitisha mtiririko wa silaha hatari za kisasa kuelekea kwa wanamgambo wa kigaidi. Lazima muwalaani wanamgambo hao, muwatambulishe kama wahalifu, muwaorodheshe kama kundi la kigaidi, na lazima mkomeshe mtiririko wa mamluki.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, katika hotuba yake ya “Hali ya Dunia” wakati wa ufunguzi wa mkutano huo alisema: “Nchini Sudan, raia wanachinjwa, wanakumbwa na njaa na wananyamazishwa,” Guterres alisema. “Wanawake na wasichana wanakabiliwa na ukatili usioweza kuelezwa.”

Naibu Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu alisema mwezi Julai kwamba mahakama inaamini uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu unatekelezwa Darfur, ambako RSF inadhibiti miji yote mikuu ya mikoa isipokuwa El-Fasher katika Darfur Kaskazini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *