Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ameonya katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa Pakistan, kuhusu malengo hatari ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kupanua vita hadi nchi nyingine za kanda ya Asia Magharibi.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, na Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, walibadilishana maoni kuhusu matukio ya kikanda na athari za uchokozi wa kijeshi uliofanywa na utawala wa Kizayuni pamoja na Marekani dhidi ya Iran, katika mazungumzo ya simu yaliyofanyika Jumamosi.

Katika mazungumzo hayo, Rais wa Iran alieleza masikitiko yake kuhusu jinsi ardhi za baadhi ya nchi za Kiislamu zinavyotumiwa katika mashambulizi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na akasisitiza: “Hatua ya Iran ya kujilinda dhidi ya chanzo cha mashambulizi haya ni jambo la kawaida. Hata hivyo, Jamhuri ya Kiislamu inazitambua nchi za Kiislamu kuwa ndugu zake, na haitaki kuona hata Mwislamu mmoja akipatwa na madhara.”

Amesisitiza pia kwamba utawala wa Kizayuni wa Israel una nia mbaya ya kupanua vita hadi nchi za kanda hii, na akaonya kuwa nchi za Kiislamu zinapaswa kuwa makini ili ardhi zao zisitumiwe na wavamizi kufanya mashambulizi dhidi ya nchi nyingine za Kiislamu.

Pezeshkian ameashiria uhusiano wa kidini na kibinadamu kati ya nchi za Kiislamu, akisema kuwa kuna uwezo mkubwa miongoni mwa nchi za Kiislamu wa kukabiliana na vitisho vya pamoja, hasa uchokozi wa utawala wa Kizayuni.

Waziri Mkuu wa Pakistan, katika mazungumzo hayo, amesisitiza tena msimamo wa kimsingi wa nchi yake wa kulaani uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran. Amesisitiza hasa kulaaniwa vikali kwa mashambulizi ya hivi karibuni ya utawala wa Kizayuni dhidi ya miundombinu ya kiuchumi ya Iran, na kutilia mkazo mshikamano kamili wa serikali na wananchi wa Pakistan na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *