Zaidi ya watoto 300 wameuawa au kujeruhiwa nchini Sudan katika kipindi cha miezi sita iliyopita, huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (drones) yakiwa chanzo kikuu cha vifo na majeraha hayo. Hayo yamefichuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kusaidia watoto (UNICEF) wakati mapigano yakizidi kuenea katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo ya Afrika.

Katika taarifa iliyotolewa na UNICEF siku ya Jumatatu, imebainika kuwa takriban asilimia 60 ya majeraha na vifo vya watoto vilivyorodheshwa katika kipindi hicho vilitokana na matumizi ya teknolojia ya ndege zisizo na rubani au droni. Shirika hilo limeeleza kuwa mzozo huo kwa sasa umejikita katika majimbo ya Kordofan, Darfur, na Blue Nile.

UNICEF imesema kuwa mashambulizi ya droni na mizinga imelenga miundombinu ya kiraia, ikiwemo shule, masoko, vituo vya mafuta, na vituo vya maji, jambo ambalo limeweka zaidi ya watu 500,000 katika hatari kubwa ya maisha. Aidha, UNICEF imebainisha kuwa raia wamekuwa wakiteseka katika hali kutokana na mzingiro wa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Sheldon Yett, mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan amesema:  “Watoto wamekwama katika mzunguko usioisha wa vurugu, ukimbizi, na ukosefu wa mahitaji ya msingi.”

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umetoa wito kwa pande zote zinazopigana katika mzozo huo “kulinda raia na miundombinu ya kiraia, kuruhusu na kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa haraka na bila vikwazo, na kuchukua hatua zote zinazowezekana kulinda watoto dhidi ya madhara.”

Sudan imezama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Aprili 2023, kati ya jeshi la Sudan na kikundi cha waasi kinachojulikana kama Jeshi la Msaada wa Haraka (RSF). Serikali ya Sudan inaituhumu serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuwa inawaunga mkono waasi hao wanaotekeleza mauji ya umati nchini humo.

Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa vitendo vya kikatili zaidi huku jeshi la Sudan na wapiganaji wa RSF wakipambana kwa nguvu ili kudhibiti mji wa kimkakati wa el-Obeid uliopo Kordofan Kaskazini.

Pia siku ya Jumatatu, Baraza la Haki za Binadamu linaloungwa mkono na Umoja wa Mataifa jijini Geneva, limeidhinisha bila kupigiwa kura, hatua ya kulaani kuongezeka kwa jinai zinazofanywa na waasi hao wa RSF pamoja na washirika wao ndani na karibu na mji wa el-Obeid.

Hatua hiyo pia inahimiza kuongezeka kwa msaada kwa nchi zinazopokea wakimbizi kutoka Sudan na inalaani “aina zote za uingiliaji kati wa nje” katika mzozo huo.

Vita hivyo hadi sasa vimeshasababisha vifo vya watu angalau 59,000, kuwafanya watu takriban milioni 13 kukimbia makazi yao, na kupelekea sehemu nyingi za Sudan kuingia katika hali ya njaa kali. Zaidi ya watu milioni 30 nchini kote wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *