
Nigeria imetangaza kwamba raia wake wawili waliuawa mwezi uliopita nchini Afrika Kusini, kufuatia wimbi la maandamano ya chuki dhidi ya wahamiaji yaliyokuwa yakilenga wafanyakazi kutoka mataifa mengine ya Afrika nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Nigeria, raia hao wa Nigeria waliuawa mnamo Juni 28, siku mbili kabla ya “muda wa mwisho” usio rasmi uliowekwa na waandamanaji hao kwa wageni kuondoka nchini humo,
Katika miezi ya Aprili na Mei, waandamanaji hao dhidi ya wageni walikuwa wakitupia lawama raia wa kigeni kwa kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira, uhalifu, na shinikizo kwenye huduma za umma. Machafuko hayo yalisababisha nchi za Nigeria, Ghana, na Malawi kuchukua hatua za haraka za kuwarejesha nyumbani raia wao, huku zikiwaita mabalozi wa Afrika Kusini kwa mashauriano ya kidiplomasia.
Kumbukumbu za mwaka 2008 zinaonyesha zaidi ya watu 60 waliuawa nchini Afrika Kusini katika kile ambacho makundi ya kutetea haki za binadamu yalikitaja kuwa ni vitendo vya chuki dhidi ya wageni (xenophobia).