Msemaji wa Kamandi ya Khatam al‑Anbia ya Jeshi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameonya kuwa uvamizi wowote wa kijeshi wa Marekani kupitia nchi kavu au jaribio la kuikalia kwa mabavu ardhi ya Iran utamalizika kwa madhara makubwa, akisema askari wa Marekani watakumbana na maangamizi na hata kugeuka “chakula cha papa” katika Ghuba ya Uajemi.

Katika taarifa, Ebrahim Zolfaqari ameionya Marekani dhidi ya jaribio lolote la kuivamia Iran kupitia operesheni za nchi kavu, akisema hatua hiyo itakuwa na matokeo ya kuaibisha kwa majeshi ya Marekani.

Ameashiria vitisho vya mara kwa mara vya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu uwezekano wa operesheni za nchi kavu na kukalia kwa mabavu baadhi ya visiwa katika Ghuba ya Uajemi, na kusema rais wa Marekani ameathiriwa na mashinikizo kutoka nje. Aidha amesema mtawala huyo wa Marekani amekuwa akichukua misimamo inayobadilika‑badilika na isiyoaminika.

Msemaji huyo amebainisha Marekani imemkabidhi jukumu la amiri jeshi mkuu mtu ambaye maamuzi yake yameyatumbukiza majeshi ya Marekani katika “kinamasi cha mauti,” ameongeza kuwa wanajeshi wa Marekani walioko katika eneo la Asia Magharibi tayari wanakabiliwa na vitisho vikubwa kila siku.

Aidha amedokeza kuwa wanajeshi wa Marekani wamelazimika kuondoka katika kambi zilizoharibiwa na kutafuta hifadhi katika maeneo ya kiraia na vituo vya kiuchumi ndani ya nchi za kanda, huku bado wakiwa wanakabiliwa na hatari ya kushambuliwa.

Akizungumzia uwezekano wa uvamizi wa nchi kavu, Zolfaqari amesema vikosi vya Iran vimejiandaa kwa muda mrefu kwa hali kama hiyo na vinasubiri kujibu. Ameonya kuwa kitendo chochote cha uchokozi au jaribio la kukalia kwa mabavu  ardhi ya kitakuwa na matokeo kama vile kukamatwa kwa wanajeshi, kusambaratika kwa vikosi vya uvamizi, na kutoweka vitani.

Ameongeza kuwa makamanda na wanajeshi wa Marekani hatimaye watageuka kuwa “chakula cha papa katika Ghuba ya Uajemi.”

Msemaji huyo pia amewataka viongozi wa Marekani wajifunze historia ya Iran na kuchukua funzo kutokana na makabiliano ya zamani na wavamizi wa kigeni, akionya dhidi ya maamuzi yasiyo ya busara ambayo yanaweza kusababisha vifo vingi miongoni mwa askari wa jeshi la Marekani.

Amehitimisha kwa kusema kuwa Vikosi vya Ulinzi vya Iran viko tayari kikamilifu na vitakabiliana kwa nguvu na jaribio lolote la uvamizi wa nchi kavu.

Marekani na utawala wa Israel walianzisha vita vya kichokozi dhidi ya Iran kwa kumuua kigaidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Shahidi Imam Khamenei, pamoja na makamanda kadhaa waandamizi wa kijeshi na raia tarehe 28 Februari sawa na tarehe 10 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Mashambulizi hayo  ambayo yangali yanaendelea yanahusisha mashambulizi makubwa ya angani dhidi ya maeneo ya kijeshi na ya kiraia kote Iran, na yamesababisha vifo vya  raia, na idadi kubwa ya watoto wadogo pamoja na uharibifu mkubwa wa miundombinu.

Katika kulipiza kisasi, Vikosi vya Ulinzi vya Iran vimetekeleza oparesheni za kulenga ngome za Marekani na Israel katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu pamoja na kambi za kijeshi zao za kijeshi katika baadhi ya nchi za eneo kwa kutumia makombora na ndege zisizo na rubani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *