WAZIRI Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba ameagiza kuanza mara moja utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 kupitia Mpango na Bajeti ya Serikali, akisisitiza ushirikishwaji wa sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kuharakisha ukuaji wa uchumi jumuishi na shindani.

Dk. Mwigulu ametoa maagizo hayo Aprili 1, 2026, Bungeni jijini Dodoma, wakati akiwasilisha hotuba ya mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali pamoja na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2026/2027.

Ameitaka Tume ya Mipango kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Dira 2050 ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau katika utekelezaji wake.Amesema Dira hiyo iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 17, 2025, inalenga kujenga Taifa jumuishi, lenye ustawi kwa wote, haki na linalojitegemea ndani ya kipindi cha miaka 25 ijayo. “Nitoe rai kwa viongozi wa Serikali, dini, sekta binafsi na asasi za kiraia kuhakikisha mipango yao inawiana na vipaumbele vya Dira 2050,” amesema.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, utekelezaji wa Dira hiyo unalenga kufikisha uchumi wa Taifa kufikia dola trilioni moja na pato la mtu mmoja mmoja kufikia dola 7,000 kwa mwaka ifikapo 2050. Ametaja nguzo muhimu za kufanikisha malengo hayo kuwa ni utawala bora, amani, usalama na matumizi bora ya rasilimali za Taifa ili kupunguza utegemezi wa nje.

Aidha, amesema Dira 2050 imejengwa katika nguzo tatu kuu ambazo ni uchumi imara, jumuishi na shindani; maendeleo ya watu na jamii pamoja na uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi. Katika utekelezaji wake, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo kuimarisha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, matumizi yenye tija ya rasilimali pamoja na kukuza utamaduni wa kuweka akiba kwa ajili ya uwekezaji.

Amesema Mpango na Bajeti ya mwaka 2026/2027 ni hatua ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/2027–2030/2031) wenye dhima ya “Mageuzi katika Kukuza Uchumi na Kuzalisha Ajira.”Pia, Serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini ili kuhakikisha uwajibikaji na utekelezaji wenye tija wa Dira hiyo.SOMA: Wabunge BLW waapishwa, wabainisha vipaumbele

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameliomba Bunge kuidhinisha shilingi trilioni 12.50 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake, ambapo trilioni 8.73 ni matumizi ya kawaida na trilioni 3.76 ni ya maendeleo. Aidha, ameomba kuidhinishwa kwa shilingi bilioni 225.02 kwa Mfuko wa Bunge, zikiwemo bilioni 207.99 kwa matumizi ya kawaida na bilioni 17.03 kwa ajili ya maendeleo.

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *