Tangu kuanza kwa mashambulizi ya Marekani na Israeli dhidi ya Iran, ukandamizaji wa nafasi ya kiraia na uhuru wa kujieleza umeongezeka kwa kiasi kikubwa kwenye eneo la  Mashariki ya Kati, ukiongeza hali ya hofu iliyokuwepo tayari kutokana na migogoro na misukosuko mingi, ameonya hii leo Kamishna Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu, Volker Türk.

Taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi ambako ni Makao Makuu ya ofisi hiyo ya  Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu inasema kuwa onyo la Kamishna Mkuu Türk linazingatia kuimarishwa kwa kiasi kikubwa kwa usalama kwenye maeneo ya kiraia, huku serikali zikiweka vikwazo vikali kwa watu wanaotekeleza haki zao za msingi za uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani.

Mathalani amesema, “wimbi la kukamatwa kwa watu, ukandamizaji, mara nyingi kwa tuhuma zisizoeleweka vizuri, vimekuwa na madhara makubwa ya kutisha watu wengi, watu ambao tayari wamekuwa wakiishi kwenye hali ya kutokuwa na uhakika, hofu na wasiwasi.”

Iran watu 2,345 wametiwa korokoroni

Nchini Iran, makadirio yanaonesha kuwa watu 2,345 wamekamatwa tangu kuanza kwa mapigano siku 32 zilizopita, wakishtakiwa kwa makosa yanayohusiana na usalama wa taifa, ikiwa ni pamoja na ugaidi, upinzani, madai ya ujasusi na kushirikiana na adui.

Türk amesema idadi kubwa ya waliokamatwa kiholela wakati wa maandamano ya mwezi Januari nchini Iran na wakati wa mzozo unaoendelea wanashikiliwa katika hali mbaya sana, na wanakabiliwa na kesi za haraka ambazo mara nyingi hazizingatii taratibu za haki na zina hatari ya hukumu ya kifo. 

Tayari mauaji ya watu wanane yamefanyika baada ya kuhukumiwa, na watu watatu kati yao wanahusishwa na maandamano. Wengine wengi waliopatikana na hatia – wakiwemo watoto – wanakabiliwa na hatma kama hiyo.

Kamishna Türk  amesema, “hili linatisha. Kana kwamba maumivu na mateso yanayosababishwa na vita hayatoshi, baadhi ya Wairani wanakusanywa kiholela, kufungwa, kushtakiwa bila kufuata taratibu za haki, na katika baadhi ya kesi hata kuuawa na serikali yao wenyewe.” Hivyo amesema, “haki za binadamu za watu wa Iran lazima ziwekwe mbele. Hukumu zote za kifo lazima zisitishwe mara moja.”

Wiki ya 5 bila intaneti nchini Iran

Wakati huo huo, hii ni wiki ya tano tangu intaneti kukatwa Iran, ikiwa ni mojawapo ya hatua za kuzimwa kwa mtandao kwa kiwango cha nchi nzima  kilicho kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa duniani. 

Ripoti zinaendelea kuonesha mahojiano ya kulazimishwa na vitisho dhidi ya raia vinavyofanywa na vikosi vya usalama vilivyo na silaha nzito katika maeneo ya umma.

Palestina, Bahrain, Qatar, Kuwait, UAE, Jordan nako uhuru wa kiraia mashakani

Huko eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu, mamlaka za Israeli zilitangaza kuwakamata Wapalestina 200 kati ya tarehe 28 Februari hadi 6 Machi, wakiwemo waliokamatwa kwa kuchapisha kwenye mitandao ya kijamii na kwa tuhuma za uchochezi na kusifu adui.

Nchini Bahrain, mwanaharakati Mohammed Al-Mousawi alifariki dunia akiwa kizuizini yasadikiwa tarehe 27 Machi, huku kukiwa na madai mazito ya kuteswa. 

Nazo Qatar na Umoja wa Falme za Kiarabu, mamlaka zimetangaza kuwashikilia watu 313 na 109 mtawalia, kuhusiana na kurekodi au kusambaza taarifa, hayo yakiwa ni miongoni mwa mashtaka mengine. 

Nchini Kuwait, amri mpya imeweka kifungo cha jela na faini kubwa kwa kusambaza taarifa zinazolenga “kudhoofisha heshima ya jeshi” au kupunguza imani ya umma kwake. Kukamatwa kunakohusiana na mzozo huu pia kumeripotiwa.

Nako Jordan, angalau wakosoaji wanne waliripotiwa kukamatwa wakati wa wimbi la sasa la uhasama, wakiwemo wanachama watatu wa Chama cha Kikomunisti cha Jordan, wawili wao bado wanazuiliwa bila sababu inayojulikana.

Waliokamatwa kiholela waachiliwe haraka

Kamishna Mkuu Türk  amesema, “tunakumbusha nchi zote wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu kuheshimu na kulinda haki ya watu ya uhuru wa kujieleza. Kila mtu ana haki ya kutoa maoni ya kukosoa, hasa kuhusu masuala muhimu ya umma, bila hofu ya kukamatwa kiholela na kuadhibiwa.”

Na zaidi ya yote “hata wanaokamatwa wana haki yao kupata wakili, kufuata taratibu za haki na kusikilizwa kwa haki. Kuwekwa kizuizini kabla ya kesi lazima iwe hatua ya mwisho, inayotumika tu pale inapohitajika. “Watu waliokamatwa kiholela lazima waachiliwe mara moja bila masharti,” ametamatisha Kamishna huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *