Mwanza. Kama ilivyo muhimu kwa binadamu kupumua ili kuishi, hali ya mwanaume kuamka asubuhi akiwa na uume uliosimama pia ni ishara muhimu ya afya ya mwili.

Wataalamu wa afya wanasema hali hiyo inathibitisha kuwa mzunguko wa damu na mfumo wa neva unafanya kazi vizuri, na ni sehemu ya mwili kuonyesha afya ya jumla.

Kwa wanaume wengi, kuamka asubuhi wakiwa na uume uliosimama ni jambo la kawaida. Hata hivyo, kuamka jogoo kalegea mara kwa mara kunaweza kuwa hatari, kwani ni ishara ya mapema kwamba mwili unaweza kuwa na tatizo fulani likiwemo mzunguko wa damu, nguvu za kiume au hata matatizo ya moyo.

Wasemavyo wataalamu

Baadhi ya wataalamu wa afya wanashauri kuwa mwanamume anayezinduka usingizini asubuhi jogoo lake likiwa legevu anaweza kuwa na matatizo ya moyo. Wanaume wengi huamka asubuhi jogoo likiwika, na likilegea linaweza kuwa ishara ya tatizo la moyo.

Kulingana na mtaalamu wa magonjwa ya moyo, Dk Adam C. Powell, kuwika kwa jogoo la mwanamume asubuhi hutokana na mtiririko mzuri wa damu kwenye mishipa ya uume.

“Mtu anapopoteza hili asubuhi, inaweza kuwa ishara ya kuzorota kwa mifumo ya mzunguko wa damu, ambayo ni ishara ya tatizo la moyo” aliliambia gazeti la Daily Mail.

Hata hivyo, inaelezwa pia kuwa kuamka uume ukiwa umelegea mara moja au mara chache hakuwezi kuashiria tatizo kubwa. Lakini pale hali hii inadumu kwa muda mrefu, ni tahadhari kwamba mwili unaweza kuwa unatoa ishara ya mapema ya matatizo ya kiafya.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika Hospitali ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk Agostino Makenya anasema hakuna jibu la ndiyo au hapana japo kuna uhusiano kati ya uume kulegea na magonjwa ya moyo.

“Kama tunavyojua kuna uhusiano wa damu na moyo kwahiyo inawezekana kwenye moyo kukawa na changamoto, kwahiyo mtu akijigundua ana hali kama hiyo ni vyema akafanye uchunguzi ili kujua shida iko wapi lakini kusema moja kwa moja kulegea kwa uume kuna uhusiano wa moyo moja kwa moja siyo mpaka aende kupima maana anaweza kuwa amelegea kwa sababu ya umri hivyo anapungukiwa nguvu za kiume,’’ anasema na kuongeza:

“Kuna ugonjwa wa kisukari kwahiyo ni vema akapima kujua shida iko wapi yawezekana kweli kwenye moyo kuna shida au siyo moyo ni nguvu za kiume zimepungua kwa sababu ya magonjwa mengine au kwa sababu ya umri,”anasema Dk Makenya.

Kazi za kitafiti

Wataalamu wa afya wamefanya tafiti kadhaa za kimataifa kuangalia uhusiano kati ya kushindwa kusimama kwa uume na matatizo ya moyo au mzunguko wa damu.

Utafiti uliofanywa mwaka 1994 uitwao Massachusetts Male Aging Study uliohusisha wanaume 1,700 wenye umri wa miaka 40 hadi 70, ulionesha kuwa wanaume waliokuwa na matatizo ya kulegea kwa uume,  walikuwa na hatari kubwa ya kupata matatizo ya moyo ikilinganishwa na wale ambao hawakuwa na tatizo hilo.

Uchambuzi wa tafiti mbalimbali (meta-analysis) uliofanywa mwaka 2010 na kuchapishwa katika Jarida la the American College of Cardiology,  ulionesha kuwa matatizo ya kusimama kwa uume  yanaweza kuonekana miaka miwili hadi mitano kabla ya dalili za moyo kuanza kuonekana, ikionyesha kwamba mwili unaweza kutoa ishara za mapema.

Pia, utafiti wa European Society of Cardiology wa mwaka 2013, uliofanywa kwa wanaume chini ya miaka 60, ulionyesha kuwa hali hiyo inawezaa kutumika kama kiashiria cha mapema cha matatizo ya mishipa ya damu hata kabla dalili za moyo kuonekana.

Mwaka 2018, utafiti uliotolewa katika Jarida la Mzunguko wa Damu uliohusisha wanaume zaidi ya 1,800, ulionesha kuwa wale waliokuwa jogoo hasimami wakiamka walikuwa na hatari kubwa ya shambulio la moyo, kiharusi au matatizo mengine ya mishipa ya damu ikilinganishwa na wale wasiokuwa na tatizo.

Hata hivyo, tafiti hizi zinaonyesha kuwa si kila mwanaume mwenye uume kulegea asubuhi ana tatizo la moyo, bali ni ishara ya kuchunguza afya kwa kina.

Sababu nyingine za jogoo kulegea

Dk Makenya anasema kuna sababu nyingi zinazoweza kuathiri hali ya uume kushindwa kusimama akitaja umri unaopunguza nguvu za kiume, ugonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na kupungua kwa homoni za kiume.

Sababu zingine ni unene kupita kiasi, matumizi ya pombe na sigara kupitiliza, msongo wa mawazo au usingizi duni.

Hatua za kuchukua mapema

Wataalamu wanashauri wanaume kufanya vipimo vya shinikizo la damu, sukari, uchunguzi wa moyo kama kuna dalili za hatari, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, kula lishe bora yenye mboga na matunda, kupunguza pombe na sigara pamoja na kudhibiti msongo wa mawazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *