
MBALI na mpango wa kusaka matokeo chanya ambao Simba itakuwa inajiandaa nao dhidi ya Azam, kocha wa kikosi hicho, Steve Barker, atakiwa kuandaa namna ya kukabiliana na mchezaji hatari zaidi kwa sasa Ligi Kuu Bara, Feisal Salum ‘Fei toto’, ametahadharishwa hilo mapema.
Takwimu zinamuonyesha kuwa Fei ambaye ametoka kuwaliza Singida Black Stars katika mchezo uliopita wa ligi ndiye mchezaji hatari zaidi kwa sasa akihusika katika mabao 12 ya Azam msimu huu, akifunga mabao saba na kutoa asisti tano, ndiye mchezaji mwenye namba kubwa zaidi.
Hivyo Barker anapaswa kuwa macho, mipango mingi ya mabao kwenye kikosi cha Florent Ibenge inapitia kwake na hata ukitazama mchezo uliopita wa Ligi ambao Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika duru la kwanza, alihusika kuamua mechi pamoja na kwamba hakuwa miongoni mwa wafungaji wa timu hiyo.
Katika mchezo huo ambao ulichezwa kwenye Uwanja wa Benjamini Mkapa, Fei alihusika katika ujenzi wa bao la kwanza.
Katika bao hilo mpira ulitoka kwa James Akaminko katikati ya uwanja, akapasiwa Fei ambaye alimwona Nassor Hamoud yupo katika nafasi nzuri katika winga ya kushoto, alimpenyezea ndani sekunde chache tayari alikuwa katika eneo la hatari ya Simba na kutoa asisti kwa Jephte Kitambala aliyekwamisha mpira huo wavuni katika dakika ya 81 kabla ya Idd Seleman Nado kufunga la pili katika dakika 88.
Mbali na mechi hiyo ukirudi nyuma katika mechi ya mwisho ya msimu uliopita kwa timu hizo kukutana, wakati wakitoa sare ya mabao 2-2, Februari 24, 2025 ilikuwa mechi yao ya kwanza mwaka jana, Fei alihusika katika mabao yote mawili ya matajiri hao wa Chamazi.
Bao la kwanza ilikuwa ni baada ya Fabrice Ngoma ambaye kwa wakati huo alikuwa akiichezea Simba alifanya makosa akiwa upande wa beki ya kulia karibu na katikati ya uwanja, Azam waliunasa mpira kwa haraka na Fei ndiye aliyepiga pasi kwa Nado ambaye naye alimpenyezea Gibril Sillah aliyepachika bao hilo.
Ilikuwa ni bao la dakika ya kwanza ya mchezo, Simba ilisawazisha katika dakika ya 25 kupitia kwa Ellie Mpanzu, wekundu wa Msimbazi walipata bao la pili katika dakika ya 75 kupitia kwa Abdulrazack Mohamed Hamza.
Wakati ambao mashabiki wa Simba wakiamini wanashinda mechi hiyo, Feisal alitoa asisti ya bao la kusawazisha kwa Azam ambalo lilifungwa na Zidane Sereri katika dakika ya 88 na mechi hiyo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
MSIKIE KOCHA
Kocha wa zamani wa Yanga, Singida United na Azam, Hans van der Pluijm amesema; “Viungo wa Simba wanatakiwa kumnyima uhuru wa kukaa na mpira mguuni, ni hatari ukimpa uhuru mchezaji wa aina yake kwa sababu anaweza kufanya maamuzi ambayo yanaweza kuwaweka katika hatari kubwa,”
“Nimeona Simba imefanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake na ipo kwenye mwelekeo mzuri na kwa staili ya uchezaji ya Azam itakuwa mechi nzuri sana ya kuitazama,” amesema kocha huyo.