Dar es Salaam. Alikiba ni tamthiliya kamili kama vile Isidingo. Inaendelea tu kila siku kila mwaka. Anachofanya ni Kuacha kazi iongee. Mashabiki wake wako ‘bize’ na ‘chalenji’ ya wimbo au ‘vesi’ yake yeye hana habari. King Kiba hajawahi kuwa na shobo kwa lolote lile.
Mgeni anaweza kukutana naye, asielewe kama aliye mbele yake ndiye King Kiba mwenye lile pini linalokimbiza mitaani. Huyu Kiba hajawahi kueleweka kama wewe siyo shabiki wake. Ana kundi la watu wanaomuelewa vile alivyo na wanampenda kufa.
Anachoimba na sauti haviakisi maisha yake. Maisha yake kama Ustaadhi, lakini anachotoa katika koromeo na maiki yake mkononi hugeuka mnyama hatari. Kuishi kama Kiba ni jukumu zito sana. Anarahisha maisha kama muziki wake anavyoufanya kama kitu fulani hivi rahisi sana.
Ukisikiliza pini zake zinakufanya usahau kama taifa linamiliki deni kubwa kuliko idadi ya raia wake. Kiba na Bien, wana bonge moja la ngoma. Bonge moja la burudani. Bonge moja la hit. Unaijeria na amapiano wameyapukutishia huko.
Kameza wapiga kelele wanaojiita wanamuziki. Kafanya kile kitu masikio ya Watanzania walitaka. Wamesahau hata bei ya mafuta kupanda wote twaimba. Watatii! Mwanamuziki hiyo ndo kazi yake. Kusoma mchezo na kuwapa raia wanachostahili.
Ni kazi ngumu sana kumuepuka shetani maisha ya sasa. Ila ni ngumu zaidi kupingana na kile alichofanya Kiba kwenye lile pini. Kuamini anaweza kufanya yeyote anachofanya Kiba, huo ni uchawi. Kiba hufanya wasichoshindwa wengine.
Muziki mzuri katika kipindi kizuri. Sikutegemea kukosa ‘unaijeria’ au amapiano katika pini jipya.
Wabongo kipindi hiki wanataka faraja. Kiba na Bien wametupa liwazo tosha kupitia ngoma yao hii. Watu tunataka vitu rahisi.
Muziki mzuri ni wenye maneno machache, yanayojirudia rudia kurahisisha hata watoto wakariri haraka. Watatii maneno yake ni machache yanayojirudia kwenye mpangilio na sauti ya viwango ambavyo TBS hawana vifaa vya kupimia.
Ogopa sana kukubalika na pisi kali. Nana Dollz yupo na Kiba. Sanchoworld yupo na Kiba. Posh Queen yupo na Kiba. Lulu yupo na Alikiba. Wote maokoto yapo hawana ‘taim’ na ‘chalenji’ wao kupenda wanachopenda hadi wapende.
Kuna wakati mambo yanatokea mpaka mtu unajiuliza hiki ni nini? Kiba na Bien wameibuka katika mazingira tatanishi kiasi kwamba huamini unachoona. Unachosikia au kukitazama. Unaweza kuona kama wimbo wa kawaida, mpaka uone pisi zinavyoshoboka.
Nilikuwa eneo fulani amazing. Eneo ambalo halina urafiki na njaa njaa. Nilienda kutumia pesa kwa vyakula visivyo na ‘kolabo’ na minyoo. Lengo nigombanishe minyoo na saladi, samosa, fileti na korekore. Nilifanikiwa.
Nilikerwa na uwepo wa visenti mfukoni vya mwisho wa mwezi.
Aina ya binadamu waliokuwepo pale ni wale ambao wanasikia tu kuna mabasi ya mwendokasi lakini hawajawahi kuisikia sauti ya mrembo anayetangaza vituo.
Ilikuwa rahisi kutambua kuwa kunawanaoishi na wanasaidia kuvuta hewa ya bure. Ngozi zao hazina uhusani na hali ya nchini yetu. Wao na njaa waliipa talaka kitambo. Ni binadamu daraja la kwanza wanaoishi dunia ya tatu.
Ni mwisho wa wiki totozi kibao na mavazi ya gharama. Nywele zao ni ‘Peruvian endi Indiani hea’, wakizirusha kila dakika. Utadhani kuna upepo mkali kumbe ni zile bwembwe za Kibiyonse mbele ya Jigga Men. Ilivutia sana kuwepo pale.
Vidani vya kutosha na simu vioo vipana kama runinga za kisasa. Zinazobandikwa ukutani kama picha za Nyerere kwenye maofisi ya serikali. Wakitumia vinywaji vya gharama, vikaratasi vya bilinzao wakivisogeza kwa vudume wao.
Baada ya msosi ‘hevi’ niliendelea kuwepo pale na kuagiza kinywaji. Kinachochangamsha ubongo na kuniondolea unyonge kwa kasi. Kinywaji ambacho kinalazimisha uamini uno sawa na Spika ama Jaji Mkuu kimaisha. Kinywaji hiki kinajua sana kuniliwaza.
Kinywaji hiki hunisahaulisha sana madeni na kunipa moyo kwamba na mimi ni binadamu. Sikuvutiwa na vinywaji na sikuwa mgeni na mazingira. Kilichofanya nibaki pake ni uwepo wa warembo na mbwembwe zao. Walivutia.
Wakati nawatazama kwa jicho la matamanio, na kuwawaza kwa ubongo wenye ufukara. Ghafla ngoma na Kiba na Bien likaitika kwa ‘dijei’. Eneo lote liliamshwa na kuzalisha fujo zisizoumiza, hili pini siyo poa. Mitaa niliyokuwepo siyo ya Bongo Fleva.
Ni mitaa ile ya ‘kantri’, ‘jazi’, rock’, salsa nk. Ila eneo lote wanaimba.
“Watatii… fainalee, watatupenda! Refariii, fainale! Puliza kipyenga” Bien kaimba na ndiye mwenye pini, lakini King Kiba kanyoosha. Hapotei kibwege, na yupo sana! Kiba ni Isidingo nyingine. Haiishi!