
Dar es Salaam. “…Weka mapenzi kando leteni hoja za msingi, ni wangapi watanipenda nikiwa sina shilingi…?” Prof Jay ndo Bongo Fleva na Bongo Fleva ndo Prof. Jay. Anapofanya jambo, siyo tu jambo lake, bali ni jambo la wanamuziki wa Bongo Fleva.
Nategemea jambo lake kubebwa na wanamuziki zaidi wa muziki wa Bongo Fleva kuliko mashabiki wa muziki wake. Jay ndo aliyewapa kurunzi la maisha ya muziki kwa wanamuziki wa muziki huu. Yes, alichonga na kusakafia barabara yote.
Prof. Jay siyo msanii wa kawaida ni alama hai ya mabadiliko na uthubutu ndani ya Bongo Flava. Yeye na muziki wamefungamana kwa namna ambayo ni vigumu kuwatenganisha. Ana haki miliki ya ‘legasi” kubwa na muziki huu.
Utake usitake.
Ndiye aliyewaambia vijana kuwa muziki chombo cha kuelimisha, kukosoa na kuhamasisha jamii. Akawaambia wazazi muziki ni ajira. Akaziaminisha kampuni, taasisi na mashirika kuwa muziki ni mdau namba moja kwa vijana na maendeleo.
Nyimbo zake zinagusa maisha ya Mtanzania wa kawaida. Kuanzia changamoto za kijamii, kisiasa na maadili. Jay alijimilikisha hati miliki ya sauti ya wasiokuwa na jukwaa. Alimsemea denti, konda, machinga, teja, dada poa, polisi, kibaka mpaka baamedi.
Prof. Jay anabaki kuwa mmoja wa walioweka msingi imara. Siyo pini zake, bali kwa ujasiri wake wa kusimamia kile anachoamini. Aligeuza muziki kuwa harakati, na harakati kuwa urithi na urithi kuwa maisha nje ya ajira zetu za miaka na miaka.
Safari hii, baada ya changamoto nyingi, anaenda kupewa heshima yake. Pengine bila madhira yake ya kiafya, angekuwa wa kwanza kupewa heshima. Kila jambo ni wakati na sasa ndo wakati sahihi zaidi kwake na muziki wenyewe. Huyu ndiyw yule…
Hili ni jambo la wanamuziki wa Bongo Fleva. Kachukue albamu zake na za wasanii wa mwanzo kati na sasa hivi. Kisha njoo na majina ya wale alilshirikiana nao kisanii ndani na nje ya sanaa. Utagundua yeye ndiye Safina ya Bongo Fleva.