Geita. Tukio la kuzaliwa kwa mbuzi mwenye viungo vya jinsia zote mbili (kike na kiume) limeibua mshangao na taharuki kwa wakazi wa Mtaa wa Nyantorotoro B, Kata ya Nyankumbu, Manispaa ya Geita, huku wataalamu wa mifugo wakilitaja kuwa ni jambo la kawaida kisayansi.
Mmiliki wa mbuzi huyo, Catherine Kachwele, mkazi wa eneo hilo, amesema alijikuta katika hali ya sintofahamu baada ya kugundua kuwa mbuzi aliyopewa kama zawadi ana jinsia mbili.
Kutokana na hali hiyo, amelazimika kumtelekeza kwa balozi wa shina ili apatiwe maombi, akiamini huenda angeweza kubadilika na kuwa na jinsia moja.
Akizungumza na Mwananchi Aprili 4, 2026, Kachwele, ambaye ni mtaalamu wa tiba asili, ameeleza kuwa alipata mbuzi huyo mkoani Kigoma kama sehemu ya malipo ya huduma ya matibabu aliyotoa kwa mgonjwa aliyekuwa hana fedha za kutosha.
Catherine Kachwele ambaye ni mmiliki wa mbuzi mwenye jinsi mbili akidaiwa kumtelekeza kwa balozi baada ya kujawa na hofu kutokana na tukio hilo ambalo ni jipya kwake.
Amesema kutokana na safari ya usiku, hakupata nafasi ya kumkagua kwa kina mbuzi huyo hadi alipowasili nyumbani Geita, ambapo alishangazwa na mkusanyiko wa watu waliokuwa wakimshangaa mnyama huyo.
“Nilipomchunguza ndipo nilibaini ana viungo vya jinsia zote mbili. Nilishauriana na baadhi ya watu, wengine wakaniambia ni hali ya kawaida na kuna mbuzi wa aina hiyo wanaoweza hata kuzaa, ingawa walisema huyu aliwahi kuzaa lakini mtoto alikufa,” amesema Kachwele.
Ameongeza kuwa alijaribu kumtafuta aliyempa mbuzi huyo bila mafanikio, kabla ya kuwasiliana na mtu aliyewaunganisha, ambaye alimweleza kuwa mnyama huyo alizaliwa katika hali hiyo na si wa kipekee.
Kwa upande wake, balozi wa shina namba 20 wa mtaa huo, Damian Mosha, amesema alipokea taarifa za kuwepo kwa mbuzi aliyefungwa porini majira ya usiku na kuamuru aletwe nyumbani kwake kwa usalama wakati mmiliki akitafutwa.
“Siku iliyofuata nilipomchunguza, niligundua ana jinsia mbili. Nilimtafuta mmiliki wake ambaye alikiri ni wake, lakini aligoma kumchukua na kuniomba nimuombee ili abadilike,” amesema Mosha.
Amesema tukio hilo ni la kwanza kushuhudiwa katika eneo hilo na kutoa wito kwa jamii kuachana na imani za kishirikina, akieleza kuwa hata kwa binadamu hali kama hiyo inaweza kujitokeza.
Akitoa ufafanuzi wa kitaalamu, daktari wa mifugo wa Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Jackson Mutayaba, amesema hali hiyo inajulikana kama hitilafu ya kuzaliwa (congenital anomaly), ambapo viungo vya mwili hujitokeza tofauti na mpangilio wa kawaida.
Ameeleza kuwa moja ya sababu zinazoweza kuchangia ni pamoja na kuzaliana kwa wanyama wa ukoo mmoja (inbreeding), hali inayoweza kusababisha mabadiliko yasiyo ya kawaida katika maumbile ya wanyama.
“Wafugaji wengi hawazingatii kanuni za uzalishaji bora wa mifugo, hivyo unakuta ndugu wanazaliana. Hii inaweza kusababisha matatizo kama haya. Ni muhimu kubadilisha madume kwa kuleta kutoka koo nyingine,” amesema Dk Mutayaba.
Ameshauri pia kuwa wanyama wenye hali hiyo wasitumike kwa uzalishaji, badala yake wahasiwe au watumike kwa matumizi mengine ili kuzuia kuendeleza hali hiyo katika kizazi kijacho.
Naye mkazi wa eneo hilo, Sijaona Kagosha, amesema tukio hilo limewapa hofu wananchi wengi, akiiomba Serikali kupitia wataalamu wa mifugo kutoa elimu zaidi ili kuondoa dhana potofu na hofu kwa jamii.
Tukio hilo limeibua mjadala mpana kuhusu uelewa wa masuala ya kisayansi katika jamii, huku wataalamu wakisisitiza umuhimu wa elimu kwa wafugaji ili kuboresha afya na uzalishaji wa mifugo nchini.