
Mkuu wa Vituo vya Kudhibiti Magonjwa Afrika (Africa CDC) amesema bara hilo linahitaji kuwekeza fedha zake lenyewe katika kukabiliana na Ebola.
“Kama mlipuko huu ungekuwa Ulaya, Marekani au bara lingine, tayari wangetengeneza chanjo na dawa,” amesema Dkt. Jean Kaseya, Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, katika makao makuu ya shirika hilo huko Addis Ababa.
Jean Kaseya ameongeza kuwa: “Wao hawaoni faida yoyote (ya kutengeneza dawa ya Ebola); si ugonjwa wao, haliwashuughulishi.., si watu wao wanaokufa, na nadhani hii pia ni kengele ya hatari kwa Waafrika. Tunahitaji kujitunza, tunahitaji kusema ni wakati wetu wa kufikiria kwa makini jinsi tunavyoweza kuanza kutengeneza dawa na chanjo ili kukidhi mahitaji yetu.”
Majanga ya kiafya ya hivi karibuni, likiwemo janga la COVID-19, yamepelekea kuzidishwa juhudi za kuongeza uzalishaji wa chanjo barani Afrika, lakini bado hakuna mafanikio makubwa yaliyopatikana. Hata hivyo Bwana Kaseya amesema hana uhakika kama chanjo itapatikana hadi kufikia mwisho wa mwaka huu.
Ameongeza kuwa kilele cha mlipuko wa Ebola bado kinatarajiwa kutokana na kasii ya mwendo wa kinyonga katika kutambua na kufuatilia watu walioambukizwa.
Jean Kaseya amesema maafisa bado wanahitaji kuwafuatilia zaidi ya watu 36,000 ambao wamekutana na watu walioambukizwa.
Mlipuko wa sasa tayari umesababisha vifo vya zaidi ya watu 200 na takriban watu 900 wamethibitishwa kuambukizwa.
Idadi ya visa halisi inaaminika kuwa kubwa zaidi kwa sababu mlipuko huo ulithibitishwa kwa kuchelewa kwa wiki kadhaa.
Jitihada za kukabiliana na virusi hivyo zimekabiliwa na changamoto kutokana na ukosefu wa chanjo au matibabu yaliyoidhinishwa ya spishi ya Bundibugyo ya virusi hiyo inavyosababisha mlipuko wa sasa.