LICHA ya timu ya Taifa ya Kabaddi Wanawake Zanzibar kushiriki mashindano ya kimataifa yaliyofanyika Bangladesh na India kutwaa taji hilo kwa msimu wa pili mfululizo, lakini bado wanawake kisiwani hapa hawajawa na mwamko kwa mchezo huo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Kabaddi Zanzibar, Ramadhan Mrisho, amesema wanawake wengi wana hofu ya kucheza mchezo huo kutokana na namna ya uchezwaji wake.

“Mchezo wa Kabaddi lazima ujitoe, hivyo wana hofu sana kwani wanaona ni kitu cha kushambuliana na kushambuliwa, hiyo ndio changamoto kubwa kwa upande wa wanawake,” amesema kiongozi huyo.

Amesema changamoto hiyo ndiyo inasababisha kuwa na mwitikio mdogo kutoka kwao ingawa wapewa nafasi kubwa ya kushiriki mchezo huo duniani.

Mbali na hilo, mwitikio wa wadau nao umekuwa mdogo kwa timu za wanawake ikizingatiwa kwa upande wa wanawake huduma zao zinatakiwa kuwa na ukaribu zaidi.

Amesema hiyo inakuwa ni tofauti na timu za wanaume na wanaweza kujikimu kwa baadhi ya mahitaji yao kwani wana uwezo wa kufanya shughuli nyingine nje ya mchezo huo.

Amesema, wapo baadhi ya wachezaji wakike wanashindwa kufika mazoezini kwa kukosa nauli, wakati mwingine hali hiyo inawakatisha tamaa.

Pia, amesema mchezo huo kwasasa hauna mdhamini wa kudumu jambo ambalo linarudisha nyuma washiriki na kulazimika kujitegemea wenyewe bila ya msaada ya mtu mwengine.

Katibu huyo ametoa wito kwa wadau kujitokeza kwa ajili ya kutoa udhamini wa mchezo huo ili kuendeleza ndani na nje ya Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *