Shirika la Umoja wa Mataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limethibitisha kwamba mashambulizi ya hivi karibuni ya kijeshi yalifanyika karibu na Kinu cha Nyuklia cha Bushehr cha Iran, huku Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) likitahadharisha kuhusu hali ya kutisha ya mashambulizi yanayoathiri vituo vya afya nchini Lebanon.
Mtambo wa nyuklia ulioko Bushehr nchini Iran.
Kulingana na taarifa ya IAEA waliyoichapisha katika ukurasa wao wa mtandao wa X, uchanganuzi wa picha za satelaiti kuanzia jana tarehe 5 Aprili unaonesha kuwa ingawa Kinu cha Nguvu za Nyuklia cha Bushehr chenyewe hakikuharibiwa, shambulio moja lilitua mita 75 tu kutoka eneo hilo. Shirika hilo limeelezea ukaribu wa athari hiyo kuwa muhimu sana, ikizingatiwa athari zinazoweza kutokea za uharibifu wowote wa miundombinu ya nyuklia. Kituo cha Bushehr ndicho kinu pekee cha nishati ya nyuklia cha Iran kinachofanya kazi na kina jukumu muhimu katika usambazaji wa nishati nchini humo.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Rafael Mariano Grossi ameonya kwamba kuendelea kwa shughuli za kijeshi karibu na mtambo huo kunaweza kuwa na athari mbaya. “Shughuli zinazoendelea za kijeshi karibu na BNPP … zinaweza kusababisha ajali mbaya ya radiolojia na matokeo mabaya kwa watu na mazingira nchini Iran na kwingineko,” amesema.
Grossi amesisitiza kwamba matukio kama hayo yanasisitiza hatari halisi kwa usalama wa nyuklia na akasisitiza kwamba vifaa vya nyuklia na maeneo yanayozunguka lazima yasilengwe kamwe.
Dhidi ya mifumo ya afya
Nchini Lebanon, WHO imeripoti kuwa takriban watu wanne wameuawa na 39 kujeruhiwa katika shambulizi la Jumapili karibu na Hospitali ya Chuo Kikuu cha Rafik Hariri, kituo kikubwa zaidi cha afya cha umma nchini humo. Ingawa hospitali yenyewe haikuharibiwa, tukio hilo limeongeza wasiwasi juu ya kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya miundombinu muhimu ya afya. WHO imethibitisha muundo endelevu wa mashambulizi dhidi ya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na matukio 11 yaliyorekodiwa kati ya 28 na 31 Machi pekee, wastani wa mawili kwa siku kote kusini mwa Lebanon na Beirut.
Jengo lenye uharibifu mkubwa linasimama huko Beirut baada ya mashambulizi ya anga ya hivi karibuni nchini Lebanon.
Tangu kuongezeka kwa ghasia kuanza tarehe 28 Februari, jumla ya mashambulizi 92 kwenye vituo vya afya, magari ya kusafisha wagonjwa, wafanyakazi na maghala yamethibitishwa, na kusababisha vifo vya 53 na majeruhi 137. Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amelaani mwelekeo huo, akisema, “vitendo hivi haviwezi kuwa kawaida mpya.” Amezitaka pande zote kuzingatia wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, akisisitiza kuwa ulinzi wa wahudumu wa afya, wagonjwa na vituo vya afya ni jukumu la wote linalopaswa kuheshimiwa wakati wote.