Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani leo kwa njia ya video kutoka mjini Havana, Cuba, Pichon amebainisha kuwa siku 10 zilizopita, Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Dharura, (OCHA), na kwa mazungumzo ya karibu na mamlaka za kitaifa, wamezindua Mpango Ulioboreshwa wa utekelezaji kupatia majawabu hali ya sasa ya dharura ya nishati na masalia ya madhara ya kimbunga Melissa.
Amesema changamoto ya nishati ina athari mbaya kibinadamu na ikigusa nyanja zote za maisha ya kila siku nchini Cuba, kuanzia afya, maji na usafi wa mazingira, mifumo ya upatikanaji wa chakula, elimu, usafiri na mawasiliano.
Mratibu Mkakazi wa Umoja wa Mataifa huko Cuba, Francisco Pichón, atembelea hospitali ya uzazi. (MAKTABA)
Je Umoja wa Mataifa unafanya nini?
Hata hivyo Pichon amesisitiza kuwa “Umoja wa Mataifa unafanya kazi kikamilifu na washirika na nchi wanachama kutafuta suluhisho ili kuhakikisha uendelevu wa shughuli zake, pamoja na kusaka wadau wengine wanaoweza kuchangia majawabu ya upatikanaji wa bidhaa ikiwemo mafuta. Na tunafanya hivi kwa kushirikiana na sekta binafsi nchini Cuba.”
Afisa huyo amesema mpango huo “umebuniwa kuunga mkono juhudi za kitaifa” na unalenga “matumizi ambayo sio tu yanaweza kufuatiliwa bali pia yanayozingatia ufinyu wa rasilimali kwa sasa na kulingana na mahitaji ya kila sekta inayolengwa; usafirishaji, afya, maji na usafi wa mazingira, uhakika wa chakula, makazi, ulinzi wa makundi yaliyo hatarini, pamoja na elimu.
‘Mazungumzo’ kati ya OCHA na Marekani
Pichon amesema kuna “mazungumzo yanayoendelea” kati ya OCHA na Marekani, “kwa msaada wa baadhi ya nchi wanachama ili kufikia muafaka utakaowezesha kupeleka mafuta Cuba ili kuitikia wito wa kibinadamu na kuhakikisha tunaweza kulinda huduma muhimu.”
Tarehe 29 Januari 2026, Marekani ilitoa amri ya kiutendaji iliyoendelea kuongeza vikwazo kwenye usambazaji wa mafuta kutoka nchi zingine kwenda Cuba.