MKAZI wa Kijiji cha Kagunguli wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Renatus Silivester ameuawa na wananchi baada ya kuingia ghafla katika Kanisa Katoliki wilayani Ukerewe kwa nia ya kumjeruhi paroko wakati waumini wakiendelea na Ibada ya Pasaka.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa amesema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika Parokia ya Kagunguli wilayani Ukerewe. Amesema kijana huyo anayesadikiwa kuwa na ugonjwa wa akili aliingia katika kanisa hilo kupitia mlango wa upande wa kulia akiwa amebeba mfuko na kuelekea moja kwa moja madhabahuni na mmoja wa waumini, alipomshtukia kutokana na mienendo yake alimtoa nje ya kanisa.
“Walipokuwa wakimhoji, kijana huyo alitoa upanga na kuwajeruhi watu wawili na kutokana na kitendo hicho, kundi la waumini na wananchi waliokuwa nje ya kanisa walimdhibiti kwa kumpiga kwa silaha za jadi na kumjeruhi sehemu mbalimbali za mwili wake,” alifafanua.
Hatahivyo, aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Costantine Bituro ambaye ni mwenyekiti wa Parokia na mkazi wa Kagunguli, aliyejeruhiwa kichwani na mikono yote na Aloyce Christopher ambaye ni mwanakwaya.SOMA: Ugomvi nyumbani, ugoni vyaongoza mauaji 2025
Kamanda Mutafungwa amesema kijana huyo alikimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Nansio kwa ajili ya kupatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata, lakini alifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini.
