
WAZIRI Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema kuwa pasaka ni kipindi muhimu kinachowakumbusha Watanzania kuishi kwa upendo, mshikamano na kudumisha amani katika jamii. Dk Mwigulu amesema hayo kwenye Tamasha la Pasaka la Mtoko na Christina Shusho lililofanyika Mlimani City Dar es Salaam.
“Amani si kwa ajili ya faida ya rais wala serikali, bali ni kwa ajili ya kila mwananchi. Pasipo amani hata shughuli ndogo kama kujitafutia kipato haziwezi kufanyika” SOMA: Dk Mwigulu: Amani ni msingi wa maendeleo

Ameeleza kuwa mnufaika wa kwanza wa amani ni mwananchi mwenyewe, kwani bila utulivu hata shughuli za kiuchumi, kijamii na ibada haziwezi kufanyika ipasavyo. Amempongeza mwimbaji wa muziki wa Injili, Christina Shusho kwa kuandaa tamasha hilo kubwa lililovuta maelfu ya waumini, akisema mafanikio yake yanaonesha kuwa lina kibali cha Mungu. “Ukiona jambo linafanikiwa kiasi hiki, ujue lina kibali cha Mungu. Serikali haitakuwa kikwazo katika mipango ya kuendeleza huduma ya injili,” alisema.