Chanzo cha picha, Getty Images
Muda wa kusoma: Dakika 4
Rais wa Marekani Donald Trump, amechapisha kwenye mtandao wake wa kijamii kuwa Marekani na Iran karibu wanafikia “tamati” katika makubaliano ya amani, na kuwa amekubali kusitisha mashambulizi kwa wiki mbili ili kuruhusu mazungumzo yafanyike.
Trump alikuwa ameipa Iran hadi Jumanne jioni saa za Marekani kufikia makubaliano, vinginevyo Marekani ifanye mashambulizi mabaya kwa kulenga miundombinu ya uchukuzi na nishati nchini humo.
Sasa ni kusubiria na kufuatilia kuona iwapo Iran itasitisha mashambulizi yake na kukubali kufungua Mlango Bahari wa Hormuz na kuruhusu meli kupita.
Hatua hii haikuwa inatarajiwa itaafikiwa hivi karibuni baada ya tishio la Trump la kuiharibu Iran na kuirudisha “enzi za kitambo”
Haijulikani iwapo tishio la Trump liliishinikiza Iran kuafikia makubaliano ya kusitisha mashambulizi ambayo awali ilikuwa imekataa. Ila lile ambalo liko wazi ni mabadiliko ya semi za Trump baada ya kuitishia Iran siku mbili zilizopita kuwa “ataiangamiza kabisa” hilo halijawahi kutokea katika historia ya Marekani.
Na iwapo makubalino ya kusitisha vita kwa wiki mbili yataleta amani ya kudumu, vita vya Iran na matamshi ya Trump, yamebadili mtazamo wa Marekani kwa dunia.
Chanzo cha picha, Getty Images
“Hii haituwakilishi sisi”
Chanzo cha picha, Getty Images
Taifa ambalo wakati mmoja lilijulikana kudumisha amani ya dunia, limetikisa utaratibu wa kimataifa. Rais ambaye anaonekana kufurahia kuvunja kanuni na desturi katika siasa za taifa lake, sasa anafanya hivyo katika jukwaa la dunia.
Wawakilishi wa chama cha Democrat walikashifu vikali matamshi ya Trump, wengi wakitaka aondolewe madarakani.
“Ni wazi kuwa maamuzi ya rais yameendelea kudorora na hafai kutuongoza” alisema mbunge Joaquin Castro kwenye ukurasa wake wa X.
Chuck Schumer seneta wa chama cha Democrat alisema kuwa kiongozi yeyote wa Reuplican ambaye hatapinga kuwa kumaliza vita dhidi ya Iran “atawajibikia madhara yote”
Wakati wengi ndani ya chama cha Republican cha Donald Trump walimuunga mkono rais huyo, uungwaji mkono huo haukufikia kiwango cha umoja kamili ambacho huwa anakipata mara nyingi.
Austin Scott, Mbunge wa Republican kutoka Georgia na mwanachama wa Kamati ya Huduma za Kijeshi ya Bunge, alikosoa vikali vitisho vya Trump kuhusu kuiangamiza Iran kabisa
“Kauli za rais hazisaidii,” aliliambia BBC, “na sikubaliani nazo.”
Seneta wa Wisconsin Ron Johnson, ambaye mara nyingi humuunga mkono Trump, alisema itakuwa “kosa kubwa sana” kwa Trump kuendelea na kampeni yake ya mashambulizi ya mabomu. Mbunge wa Texas Nathaniel Moran aliandika kwenye mtandao ya kijamii kwamba haungi mkono “uharibifu wa Iran.”
“Hili halituwakilishi,” aliandika, “na halilingani na misingi ambayo imeiongoza Marekani kwa muda mrefu.”
Seneta wa Alaska Lisa Murkowski, ambaye mara nyingi amejitenga na rais, aliandika kwamba tishio la rais “haliwezi kuhalalishwa kama jaribio la kupata nguvu zaidi katika mazungumzo na Iran.”
Hata hivyo, White House huenda ikajibu kwamba mbinu hiyo ilifanikiwa.
Katika ujumbe wake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Truth Social akitangaza kusitishwa kwa mapigano, Donald Trump alidai kwamba Marekani ilikuwa “imetimiza na hata kuzidi” malengo yake yote ya kijeshi kwenye vita hivyo dhidi ya Iran.
Si suluhu ya kudumu
Chanzo cha picha, EPA
Jeshi la Iran limedhoofishwa pakubwa. Ingawa utawala wa Kiislamu bado uko madarakani, viongozi wake wengi wameuawa.
Ila malengo ya Marekani katika vita hivyo ni ya kutilia shaka. Hatma ya madini ya Urani na mpango wa nyuklia wa Iran bado haijulikani. Taifa hilo bado lina ushawishi wa makundi yenye silaha ukanda huo kama wahouthi wa Yemen.
Na iwapo Iran itafungua mlango bahari wa Hormuz bila masharti yoyote ya kutaka meli kulipa ada zaidi, uwezo wake wa kudhibiti mlango huo muhimu wa bahari umebainika wazi.
Katika taarifa baada ya Marekani kutangaza kusitisha mashambulizi, Waziri wa mambo ya nje wa Iran Seyed Aragchi alisema kuwa “Iran itasitisha mashambulizi yake ya kujilinda na kufungua mlango bahari wa Hormuz” aliongezea kuwa Marekani imekubali mapendekezo yenye vipengele kumi ya Iran kumaliza vita hivyo.
Mpango huo unajumuisha jeshi la Marekani kuondoka katika ukanda huo, kuondolewa vikwazo kwa Iran, fidia ya vita, na kuruhusu Tehran kuendelea kudhibiti mlango bahari wa Hormuz.
Haijulikani iwapo Trump atakubali mapendekezo haya yote na huenda mchakato wa mazungumzo ukawa mrefu.
Ila kwa sasa hii inawasilisha ushindi wa kisiasa kwa Trump, alitoa onyo kali ambalo limezaa matunda. Ila kusitisha mapigano kwa muda si suluhu ya kudumu.
Athari ya muda mrefu ya vita hivi bado haijatathminiwa.