RAIS wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amekutana na kufanya mazungumzo na Rais mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika (AU) kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu.
Mazungumzo hayo yamefanyika Jumanne, Aprili 7, 2027, katika Ikulu ndogo ya Nakasero jijini Kampala, Uganda. Katika kikao hicho, viongozi hao walijadili hali ya kisiasa na kiusalama nchini Sudan Kusini, wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo ya amani na maridhiano miongoni mwa pande zinazohusika ili kurejesha utulivu wa kudumu.

Museveni amemweleza Kikwete kuwa Uganda itaendelea kuunga mkono juhudi zote za kuleta amani nchini Sudan Kusini. Amebainisha kuwa utulivu wa nchi hiyo, hususan katika eneo la Equatoria lenye idadi kubwa ya raia wa Uganda, ni muhimu kwa usalama wa kikanda na ustawi wa kiuchumi.
Kwa upande wake, Dk. Kikwete ameeleza dhamira ya Umoja wa Afrika kuimarisha juhudi za upatanishi na utatuzi wa migogoro katika ukanda huo. Hivi karibuni, Kikwete ameteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, jukumu linalolenga kuimarisha ushirikiano wa kikanda pamoja na kusukuma mbele ajenda ya amani katika eneo hilo linalokabiliwa na changamoto za kisiasa na kiusalama.