Manchester, England. Meneja wa Manchester City, Pep Guardiola, amesema aliwaambia wachezaji wake watulie baada ya kuona Arsenal wakipoteza mchezo wao dhidi ya Bournemouth, ili kuepuka presha isiyo ya lazima.

Man City wamekuwa katika kiwango bora tangu Januari, wakishinda mechi dhidi ya Arsenal, Liverpool na Chelsea bila kuruhusu bao lolote.

Guardiola amesema kikosi chake kina morali ya ushindani inayoweza kuwafanya wapindue matokeo ya mbio za ubingwa.

“Ninawasukuma wachezaji na wao wananisukuma. Ukifika hatua za mwisho wa msimu ukiwa bado unapigania mataji, inaonyesha timu ni bora,” amesema Guardiola.

Man City sasa wamepunguza pengo hadi pointi sita nyuma ya vinara Arsenal huku wakiwa na mchezo mmoja mkononi. Timu hizo zinatarajiwa kukutana wiki ijayo katika dimba la Etihad.

Guardiola, ameongeza kuwa mchezo wao dhidi ya Arsenal wiki ijayo umegeuka kuwa kama fainali katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.

Kocha huyo amesema licha ya umuhimu wa mchezo huo dhidi ya Arsenal, bado kuna michezo mingine migumu mbele yao.

“Arsenal ni kama fainali, lakini bado tuna michezo mingine migumu. Heshima niliyonayo kwa Arsenal ni kubwa sana. Wamekuwa timu bora nchini na barani Ulaya kwa kipindi hiki,” alisema Guardiola.

Ameongeza kuwa kuifunga Arsenal si kazi rahisi, hasa kutokana na uimara wao msimu huu chini ya kocha Mikel Arteta.

Kwa upande mwingine, kocha wa Chelsea Liam Rosenior amekiri kuwa yuko chini ya presha kufuatia matokeo mabaya ya timu hiyo, ambayo imepoteza mechi tatu mfululizo bila kufunga bao.

Rosenior amesema ana imani anaweza kujenga timu imara ikiwa atapewa muda wa kufanya hivyo, akisisitiza kuwa klabu hiyo ina historia kubwa inayohitaji matokeo ya haraka.

Beki wa Man City, Marc Guehi wakati akifunga bao la pili katika mechi ya LIgi Kuu England dhidi ya Chelsea. Picha na Mtandao

“Nahitaji kushinda sasa. Hii ni klabu kubwa na ninajua matarajio yake. Lakini pia ninaamini nikipewa muda tunaweza kujenga kitu imara,” amesema.

Amegusia pia kurejea kwa Enzo Fernández, ambaye alikuwa akisumbuliwa na adhabu ya ndani ya klabu, akisema atakuwa nyongeza muhimu kwa kikosi hicho.

Chelsea wanatarajiwa kushuka dimbani dhidi ya Manchester United katika mchezo ujao wa Ligi Kuu England, huku wakihitaji ushindi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *