
DODOMA: Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Catherine Joachim, amesema kuwa takwimu za utafiti uliofanyika mwaka 2022 zinaonesha kuwa maambukizi mapya ya UKIMWI nchini yanafikia watu takribani elfu 56 kwa mwaka.
Ameeleza kuwa, kwa mujibu wa taarifa hiyo, asilimia 70 ya wanaopata maambukizi mapya ni vijana wa kike, hali inayoliweka kundi hilo katika hatari ya kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.
Catherine alitoa takwimu hizo bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Kutokana na hali hiyo, Mbunge huyo alishauri kuwepo kwa mikakati ya kuwaongezea uwezo vijana wa kike ili waweze kujitegemea zaidi, akibainisha kuwa gharama kubwa za matibabu ya UKIMWI ni changamoto inayohitaji kuangaliwa kwa umakini.
”Dawa za UKIMWI gharama yake laki tano na nusu kwa mwaka hivyo ukiangalia kwa sasa hivi katika hotuba ya Waziri Mkuu inaonyesha takribani watu milioni moja na nusu wanahitaji dawa hizo za kufubaza virusi vya UKIMWI hivyo kama nchi tunahitaji zaidi ya bilioni mia nane kugharamia matibabu hayo, nilikuwa naushauri wa kisera kwanza kuongeza vyanzo ili kuweza kujitegemea zaidi cha pili kuweza kuwa na mkakati maalum wa kinga ili kuweza kuzuia vijana wetu wakike kupata UKIMWI”. amefafanua Catherine.
Ameongeza kuwa ni wakati sasa wa kufungamanisha huduma za UKIMWI katika bango kitita cha mafao cha fuko wa bima ya afya kwa wote.