Serikali ya Ujerumani imesema itaanza mazungumzo moja kwa moja na viongozi wa Taliban mjini Kabul kuhusu urejeaji wa raia wa Afghanistan waliopo Ujerumani. Waziri wa Mambo ya Ndani Alexander Dobrindt alisema lengo ni kuhakikisha wahalifu na watu wanaotajwa kuwa hatari za kiusalama wanarejeshwa mara kwa mara.

Kwa mujibu wa wizara yake, maafisa wa ndani wanatarajiwa kusafiri hadi Kabul mwezi Oktoba kwa mazungumzo ya moja kwa moja na wawakilishi wa Taliban. Hii ni mara ya kwanza Berlin kukiri kuzungumza moja kwa moja na kundi hilo, jambo linaloibua mijadala mikali.

Dobrindt alisisitiza kuwa hadi sasa mazungumzo yalikuwa ya “kiufundi” bila kueleza mahali yalipokuwa yakifanyika. Hatua ya sasa inatazamwa kama hatua ya kisera inayoweza kuathiri uhusiano wa kidiplomasia, ingawa Ujerumani haina uhusiano rasmi na Taliban.

Taliban walirudi madarakani Agosti 2021 na wameendelea kutengwa kimataifa kutokana na tuhuma za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, hasa dhidi ya wanawake na wasichana. Licha ya hali hiyo, serikali ya Ujerumani inataka kushirikiana nao kuhusu urejeaji wa raia wa Afghanistan.

Afghanistan | Wakimbizi wa Afghanistan waandamana nchini Ujerumani
Wakimbizi wa Afghanistan wakiihimiza Ujerumani itimize ahadi zake.Picha: DW

Wapinzani wakosoa vikali

Tangu kundi hilo kurudi madarakani, Ujerumani imefanikiwa mara mbili tu kuwarejesha raia wa Afghanistan kwa msaada wa Qatar. Agosti 2024, wafungwa 28 waliokuwa wametiwa hatiani walirudishwa Kabul. Julai mwaka huu, wanaume 81 waliokuwa na rekodi za mauaji, uhalifu wa kingono na dawa za kulevya pia walirudishwa.

Vyama vya Kijani na cha Mrengo wa Kushoto (Die Linke) vimepinga kwa nguvu hatua ya Dobrindt. Marcel Emmerich kutoka chama cha Kijani alisema makubaliano na Taliban ni sawa na “kuihalalisha taasisi ya Kiislamu yenye rekodi ya kigaidi,” akisema ni matusi kwa wale wote waliopigania demokrasia dhidi ya Taliban.

Clara Bünger wa chama cha Die Linke aliwaambia wanahabari kwamba “anayekaa meza ya mazungumzo na Taliban anahalalisha magaidi.” Aliongeza kuwa mpango wa kuandaa urejeaji mkubwa ni sawa na kushirikiana na utawala unaotekeleza mateso, viboko na adhabu za hadharani kila siku.

Hata hivyo, Alexander Throm, mbunge kutoka chama cha kihafidhina na mshirika wa karibu wa Dobrindt, ameupongeza mpango huo. Anasema wakimbizi wanaohukumiwa kwa uhalifu nchini Ujerumani lazima waondoke mara baada ya kutumikia vifungo vyao, bila kujali wanatoka Syria au Afghanistan.

Kwa mujibu wa Throm, njia pekee ya kulinda mfumo wa hifadhi ya wakimbizi ni kuondoa mara moja wale wanaoupotosha kwa uhalifu. Alisisitiza kuwa ni haki ya Wajerumani kulindwa dhidi ya wahalifu wanaotumia mfumo huo vibaya.

Ujerumani Munich 2017 | Maandamano dhidi ya urejeaji wa Waafghanistan kwenye uwanja wa ndege
Maandamano dhidi ya urejeaji wa Waafghanistan kwenye uwanja wa ndegePicha: Sachelle Babbar/ZUMA/picture alliance

Mustakabali wa mazungumzo

Wachambuzi wanasema mazungumzo ya Ujerumani na Taliban yataibua mjadala mpana wa kimaadili na kisiasa barani Ulaya. Swali kuu ni kama mazungumzo hayo yanamaanisha hatua ya kwanza kuelekea utambulisho wa kisiasa kwa Taliban.

Wapinzani wanatahadharisha kuwa makubaliano yoyote yatavunja misingi ya sera ya haki za binadamu ya Ujerumani, huku serikali ikisisitiza kuwa yanalenga tu wahalifu.

Hali ya usalama nchini Afghanistan bado ni tete, huku mashirika ya haki za binadamu yakiripoti vitendo vya mateso na hukumu za kikatili kutoka kwa Taliban.

Lakini kwa Ujerumani, changamoto ya kusimamia maelfu ya wakimbizi wa Afghanistan inaonekana kuishinikiza serikali kufanya maamuzi magumu hata kwa gharama ya kisiasa.

Kwa sasa, macho yote yataelekezwa Oktoba wakati maafisa wa Ujerumani watakapowasili Kabul kwa mazungumzo, hatua itakayoonyesha kama sera hii mpya inaweza kufanikishwa bila kugusa kanuni za maadili za Berlin.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *