Karibu watu 200 waliotekwa nyara na waasi wa ADF wameachiliwa huru katika siku mbili zilizopita katika eneo la Mambasa mkoani wa Ituri, kutokana na operesheni za kijeshi zinazoendelea kufanywa na Vikosi vya Wanajeshi wa DRC (FARDC) na washirika wao wa Uganda, UPDF, kulingana na wanaharakati wa mashirika ya kiraia katika eneo hilo siku ya Ijumaa, Aprili 17.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Mateka hawa walikamatwa mwezi Machi mwaka huu wakati wa mashambulizi kadhaa yaliyofanywa na kundi hilo lenye silaha la ADF katika vijiji zaidi ya kumi katika eneo hilo, kulingana na Radio OKAPI.

Jeshi la Kongo lilithibitisha kuachiliwa kwa mateka hawa, bila kutoa maelezo zaidi.

Kulingana na mashirika ya kiraia, mateka wengi waliachiliwa  tangu Jumatano ya wiki hii, hasa katika maeneo ya Bandibwame na Babungbe, takriban kilomita thelathini kutoka mji wa Mambasa.

Kwa jumla, mateka 144 wa zamani wameripotiwa kujisalimisha kwa FARDC (Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo), huku wengine zaidi ya 50 wakifanikiwa kutoroka wakati wa operesheni za kijeshi, kulingana na smashirika ya kiraia. Watu hawa wa mwisho wamejiunga na familia zao ama huko Mambasa au katika baadh ya maeneo ya mkoa wa Kivu Kaskazini.

Takriban watu 400 wametekwa nyara tangu mwezi Machi

Kulingana na mashirika ya kiraia nchini DRC, karibu watu 400 wametekwa nyara na ADF (Allied Democratic Forces) tangu katikati ya mwezi Machi katika vijiji kadhaa, ikiwa ni pamoja na Makoko, Muchanga, Bandibwame, Pumuzika, Manya, Mabukulu, na Lumalisa.

Inaripotwa kwamba kuna watu 100 ambao bado wako mikononi mwa watekaji nyara.

Kutokana na hali hii, mashirika ya kiraia yanatoa wito kwa vikosi vya pamoja vya FARDC-UPDF kuendelea na operesheni hadi ngome za ADF zivunjwe.

“Tunahimiza hatua hii ya ujasiri ya muungano iendelee, ili kvunja  ngome zote za ADF. Hii itawezesha mateka wote waliobaki kuachiliwa,” alitangaza Marie-Noelle Anotane, kiongozi wa mashirika ya kiraia huko Mambasa.

Watu wengi wameuawa

Tangu mashambulizi yaliyoanzishwa na ADF mnamo Machi 8 katika eneo la Mambasa, angalau watu 100 wameuawa, maelfu zaidi wamelazimika kukimbia makazi yao, na uharibifu mkubwa umeripotiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *