
Dar es Salaam. Katika mechi 11 zilizobaki ili kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara 2025-2026, kipa wa Pamba Jiji, Yona Amosi, anahitaji kukusanya clean sheet nne tu ili kufikia rekodi yake ya msimu uliopita, huku mwenyewe akisema anapambania kufanikisha hilo.
Amosi ambaye msimu uliopita alimaliza na clean sheet 11 katika Ligi Kuu Bara akiwa na kikosi hicho, hivi sasa anazo saba, jambo ambalo alisisitiza licha ya ugumu wa mechi zilizobaki, lakini anaamini katika kujituma hakuna linaloshindikana.
“Ingawa mechi ni ngumu, bado nina nafasi na imani kubwa kuzifikia clean sheet 11 za msimu uliopita, sifanyi pekee yangu, ni kwa ushirikiano wa timu nzima pamoja na maelekezo ya benchi la ufundi kutupa mbinu kila wakati,” alisema Amosi.
Kipa huyo aliongeza kwamba: “Pia nawafuatilia makipa wengine wanafanya kitu gani, mfano Patrick Munthali wa Mashujaa ni kipa mzuri sana, haijalishi msimu huu ana clean sheets chache, nachukua kinachonifaa kutoka kwake.”
Kwa upande wa Munthali ambaye msimu uliopita ndiye aliyeongoza kwa makipa wazawa wenye clean sheet nyingi ambazo ni 12, hivi sasa ana tatu huku akisema anayeona atazifikia rekodi zake ni Amosi aliye na muendelezo mzuri.
“Amosi kajitahidi kuendeleza kile alichokifanya msimu uliopita, sina maana kwamba kipa mwenzangu Erick Johola hafanyi vitu vikubwa, ndiye anayeongoza kwa kuwa na cleansheets sita katika timu na msimu uliopita alikuwa na mbili, ila nazungumzia ambao msimu wa 2024-2025 tulimaliza na nyingi,” alisema.
Hivi sasa kinara wa clean sheet ni Djigui Diarra wa Yanga mwenye kumi, akifuatiwa na Aishi Manula na Jean-Noel Amonome wa TRA United ambao kila mmoja anazo tisa. Msimu uliopita kinara alikuwa Moussa Camara wa Simba aliyemaliza na 19 akifuatiwa na Diarra (17).