Mbeya. Baada ya kuachana na Mecky Maxime, Mbeya City imemrejesha kikosini Salumu Mayanga kuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo.

Mayanga anarejea baada ya kuachana nao mwishoni mwa msimu uliopita alipokuwa akiiingoza wakati timu hiyo ikiwa ligi ya Championship baada ya kupata ofa kwa Mashujaa FC.

Kocha huyo anakuwa kocha wa tatu kuifundisha City msimu huu baada ya kutanguliwa na Malale Hamsini aliyepanda nao Ligi Kuu kisha Maxime aliyeachana nao ikiwa ni muda mfupi kupokea kipigo cha aibu cha mabao 6-0 dhidi ya Yanga.

Mayanga anajiunga na timu hiyo inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya akiwa huru kufuatia kuachana na Mashujaa na kibarua kizito ni kuinusuru City kutoshuka daraja.

Kwa sasa Mbeya City imebakiza michezo 11 kuamua hatma yake ya kubaki au kushuka daraja, hivyo Mayanga itamfanya kutumia uwezo, uzoefu na mbinu zote kuendelea kulinda heshima yake katika medani za soka.

Kwa sasa Ligi Kuu imesimama kupisha michuano ya kombe la Muungano, ambapo itarejea Aprili 30 ikiwa City itakuwa nyumbani kukipiga dhidi ya Mashujaa kabla ya kuwavaa ndugu zao Tanzania Prisons.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *