KIUNGO wa kimataifa wa Zambia, Larry Bwalya sasa yuko hatua za mwisho kujiunga na Pamba Jiji baada ya pande zote kufikia makubaliano kutokana na sakata la awali lililokuwa limekwamisha dili hilo.

Mwanzoni mwa msimu huu, dili hilo lilikumbwa na dosari baada ya kubainika Bwalya bado alikuwa na mkataba unaomfunga na Napsa Stars FC, jambo lililozua sintofahamu kuhusu uhalali wa usajili wake.

Hali hiyo ililazimisha Pamba Jiji kusitisha mchakato wa usajili huku wakianza kutafuta suluhisho la kisheria ili kuepuka mgogoro na klabu hiyo ya Zambia.

Inaelezwa, wakati wa sintofahamu hiyo, tayari kulikuwa na makubaliano ya awali kati ya Pamba Jiji na mchezaji huyo na alishapatiwa sehemu ya fedha zake za usajili.

Baada ya mazungumzo ya kina kati ya pande husika, sasa imefikiwa makubaliano yatakayomruhusu Bwalya kujiunga rasmi na Pamba Jiji mara tu atakapomaliza mkataba wake na Napsa Stars.

Makubaliano hayo yanaondoa uwezekano wa mgogoro wa kisheria na kufungua njia ya uhamisho huo kukamilika kwa utaratibu sahihi.

Kwa mujibu wa taarifa, kiungo huyo anatarajiwa kutua katika kikosi cha Pamba Jiji mwanzoni mwa msimu ujao.

Aidha, imeelezwa mara atakapojiunga rasmi, atalipwa kiasi kilichosalia cha fedha zake za usajili kukamilisha makubaliano yao.

Uongozi wa Pamba Jiji unaamini ujio wa Bwalya utaongeza ubora mkubwa katika safu ya kiungo na kuipa timu ushindani zaidi.

Endapo kila kitu kitaenda kama ilivyopangwa, nyota huyo atakuwa sehemu ya kikosi cha Pamba Jiji kitakachoshiriki Ligi Kuu Bara msimu wa 2026-2027.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *