BAKARI Shime ambaye ni Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Tanzanite Queens, ameita kikosi cha wachezaji 27 kinachoingia kambini kujiandaa na michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia 2026 dhidi ya Cameroon, huku JKT Queens ikionekana kutawala kikosi hicho kwa kutoa jumla ya wachezaji kumi.

Mbali na JKT Queens, pia klabu nyingine zilizotoa wachezaji wengi ni Simba Queens na Fountain Gate Princess ambazo kila mmoja ina wanne, huku Yanga Princess wakiwa watatu na Mashujaa Queens wawili. Bunda Queens, Alliance Girls na Tausi zimetoa mmoja mmoja.

Pia katika kikosi hicho, kuna nyota mmoja pekee anayecheza nje ya nchi ambaye ni Hasnat Ubamba anayekipiga FC Masar ya Misri.

Kwa mujibu wa ratiba, Tanzanite Queens itacheza michezo miwili ya kufuzu Kombe la Dunia Wanawake chini ya miaka 20, mechi ya kwanza itapigwa Mei 2, 2026 nchini Cameroon na marudiano Mei 10, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Akizungumza baada ya kutaka kikosi hicho, Shime amesema: “Tunakwenda kujiandaa na mechi dhidi ya Cameroon. Tumepata kikosi chenye uwiano mzuri wa uzoefu na vipaji chipukizi. Lengo letu ni kujiandaa vizuri ili kuhakikisha tunapata matokeo chanya dhidi ya Cameroon.”

Hii ni raundi ya nne ya kufuzu Kombe la Dunia ambapo Tanzanite Queens ilianzia raundi ya pili ya michuano hiyo kwa kuvaana na Angola na kupata ushindi wa jumla ya mabao 7-0 baada ya awali kushinda 4-0, kisha kumalizia 3-0, ikakutana na Kenya.

Katika mechi ya kwanza ugenini, ililala bao 1-0, kisha juzi kupindua meza ikiwa nyumbani na kusonga mbele kwa penalti 3-1, hivyo inakabiliana na mfupa mgumu wa Cameroon iliyoing’oa Botswana kwa jumla ya mabao 5-1, ili kukata tiketi ya kwenda Poland kushiriki Kombe la Dunia Wanawake chini ya miaka 20.

JK 01

Ratiba ya mechi zingine za raundi ya nne na ya mwisho inaonyesha Ghana itavaana na Uganda, Ivory Coast dhidi ya Benin na Nigeria kumalizana na Malawi.

Washindi wa mechi hizo nne watafuzu Kombe la Dunia, huku Tanzania ikisaka ushiriki wa mara ya kwanza kwa timu hiyo ya U20.

Wachezaji wa JKT Queens walioitwa ni Winfrida Castro, Ester Maseke, Lidya Maximilian, Aliya Fikiri, Jamila Rajab, Yasinta Mitoga, Winfrida Gerald, Zulfa Makau, Sarah Joel na Christer Basil.

Fountain Gate Princess wapo Nusrat Jaffar, Mary Siyame, Neema Paul na Hellena Hamis. Simba Queens kuna Asha Omary, Zawadi Hamisi, Elizabeth Joseph na Neema Mtunzi. Kwa Yanga Princess ni Diana Mnally, Harrier Juma na Yasinta Michael.

Wengine ni Hasnat Ubamba (FC Masar – Misri), Bahati Steven (Bunda Queens), Rhobi Daudi (Alliance Girls), Fatuma Hamisi (Tausi FC), Zuhura Mlekwa na Veronica Mapunda wote wanacheza Mashujaa Queens.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *