
BEKI wa kati wa Tanzania Prisons, Mkongomani Heritier Lulihoshi amesema bado hajajua hatma yake katika kikosi hicho, huku mkataba wake wa mwaka mmoja aliousaini na timu hiyo ukifikia tamati mwishoni mwa msimu huu wa 2025-2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lulihoshi amesema hadi sasa hakuna mazungumzo mapya ya kuongeza mkataba, ingawa lengo lake ni kuhakikisha kwanza yeye na wachezaji wenzake wanaipambania timu hiyo ili kuepuka kushuka daraja.
“Ni kweli mkataba wangu unamalizika mwishoni mwa msimu huu, ila kwa hali ilivyo ya timu ni ngumu kuzungumzia hilo kwa sasa, suala la kubakia au kuendelea nao itategemea na mazungumzo yetu yatakavyokuwa baada ya kukaa chini,” amesema Lulihoshi.
Beki huyo aliyetua Prisons Agosti 19, 2025 akitokea Dodoma Jiji iliyomsajili baada ya kuachana na Tabora United kwa sasa TRA United, amesema kutokana na presha iliyopo katika kikosi hicho ni ngumu kuanza kujadili mikataba mipya.
“Nafasi tuliyopo katika msimamo wa Ligi Kuu ni wazi tunahitaji kupambana zaidi ili kutoka chini tulipo, hata viongozi ni wazi sio rahisi kuangalia mkataba wa nani unaisha na kumwongezea, hivyo, nawaelewa kwa hiki kinachoendelea,” amesema.
Nyota huyo alianzia akademia za CPFO Goma, Bresil A.C. de Goma na Olympic Club Muungano za DR Congo, kisha baada ya hapo alizichezea ZESCO United (Zambia), Olympic Star Muyinga FC (Burundi), Musanze FC (Rwanda) na OC Bukavu Dawa ya DR Congo.
Beki huyo anaipambania Prisons ili iepuke janga la kushuka daraja na hadi sasa inashika nafasi ya 15 na pointi 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kushinda mechi tatu, sare tano na kupoteza 11, kati ya 19, ikifunga mabao 10 na kuruhusu 23.