HATIMAYE Mlandege FC imefanikiwa kuivalisha nguo Ligi ya Zanzibar, baada ya kuitupa nje ya mashindano ya Kombe la Muungano, Singida Black Stars kwa ushindi wa mabao 2-1.
Ikitokea nyuma, Mlandege imefanikiwa kusawazisha bao na kutengeneza ligine kwwenye mchezo wa robo fainali uliokuwa mkali kwa dakika zote 90, ukipigwa leo Aprili 23, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Singida ilianza mechi hiyo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya tisa tu mfungaji akiwa Mishamo Daudi, akifunga kwa kichwa akimalizia pasi ya beki, Kennedy Juma, shambulizi lililotokana na kona.
Mlandege haikuwa vibaya baada ya kuruhusu bao hilo ikatulia na kuendelea kucheza soka la kasi kwa mashambulizi ya kushtukiza ikitengeneza mashambulizi makali kwenye lango la Singida.
Mshambuliaji Mussa Hassan ‘Mbape’ almanusura aisawazishie Mlandege akishindwa kumalizia nafasi shuti lake likizuiwa vizuri na beki Rahim Shomari na kuwa kona ambayo hata hivyo haikuwa na madhara.
Mlandege ikafanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 26, mshambuliaji Omar Juma akimfunga kwa ufundi kipa wa Singida, Amas Obasogie akipokea pasi safi kutoka kwa kiungo Jamal Saleh.
Bao hilo likaendelea kuipa nguvu Mlandege na kuongeza mashambulizi lango la Singida.
Mlandege ikafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 45 mfungaji akiwa Mbape akimalizia vizuri kwa mguu wa kulia akipokea pasi ya yuleyule Saleh.
Kipindi cha pili Singida ikaingiza mastaa wake wawili, Lamine Jarjou na beki Ande Kofii ikilenga kuongeza mashambulizi na baadaye kuwaongeza washambuliaji wawili, Horso Muaku na Idris Diomande lakini hawakufanikiwa kusawazisha bao hilo na matokeo hayo kudumu mpaka mwisho wa mchezo.
Matokeo hayo yanaifanya Mlandege kuwa timu ya kwanza kutoka Zanzibar kutinga nusu fainali ya Kombe la Muungano, ikisubiri mshindi kati ya Mafunzo na Simba utakaochezwa baadaye saa 2:15 usiku.