Dodoma. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na namna ambavyo Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) unatekeleza miradi ya kusambaza nishati vijijini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema hayo Aprili 22, 2026, alipotembelea banda la Rea kwenye maonyesho ya Wiki ya Nishati 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Bunge, jijini Dodoma.
“REA mmeibeba vyema ajenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha nishati safi ya kupikia inawafikia wananchi wengi wa vijijini,” amesema Mgalu.
Amesisitiza kuwa uhamasishaji na elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia iendelee kutolewa ili kufanikisha lengo la Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema kamati anayoiongoza, pamoja na wabunge, wataendelea kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwani tayari wana uelewa wa kutosha.
Kuhusu suala la usambazaji wa umeme, Mgalu amesema kazi kubwa imetekelezwa na Rea, kwani tayari vijiji vyote nchini vimefikishiwa umeme, na kwamba miradi inaendelea kutekelezwa ya kufikisha umeme vitongojini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (Rea), Balozi Meja Jenerali mstaafu, Jacob Kingu akipata maelezo ya teknolojia iliyoboreshwa ya majiko yanayotumia mkaa maarufu majiko banifu kutoka kwa Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji wa Miradi kutoka Rea, Mhandisi Emanuel Yesaya alipotembelea Banda la Rea kwenye maonyesho ya Wiki ya Nishati 2026 yanayofanyikia katika Viwanja vya Bunge Jijini Dodoma
Kwa nyakati tofauti, wabunge waliotembelea banda la Rea walieleza kuridhishwa kwao na hatua za utekelezaji wa miradi inayoendelea kuchukuliwa na Rea.
Katika hatua nyingine, mbunge wa Sikonge, Amos Maganga, amesema Rea inafanya kazi kubwa; miradi iliyotekelezwa kote nchini imechagiza ukuaji wa uchumi vijijini pamoja na kuboresha huduma za jamii katika maeneo husika.
Maganga, aliyewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Rea, amesema kwa sasa hakuna tofauti kati ya vijiji na miji, kwani kupitia miradi iliyotekelezwa na Rea, huduma muhimu, ikiwemo za afya na elimu, kote zinapatikana kwa ubora sawa.
Aidha, wakizungumza kwa nyakati tofauti, wabunge waliotembelea banda la REA walimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Rea, Hassan Saidy, kwa uongozi wake ambao walisema umeleta chachu katika utekelezaji wa miradi.