Hai. Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amemwombea msamaha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, akiwataka wananchi wa Hai kumsamehe huku akisisitiza kuwa hakuna binadamu asiye na dhambi.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo Aprili 23, 2026, walipokutana katika mazishi ya mama wa Mbunge wa Jimbo la Hai (CCM), Saashisha Mafuwe, yaliyofanyika katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Uduru, Kata ya Machame Kaskazini.

Mwaka 2021, Sabaya alishtakiwa kwa makosa mbalimbali, ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka, utakatishaji fedha, kujipatia fedha kwa njia ya rushwa pamoja na uhujumu uchumi, alipokuwa mkuu wa wilaya hiyo.

Akizungumza katika mazishi hayo, Mbowe amesema: “Nilipofika hapa nilimkuta Sabaya akizungumza. Sabaya ni mdogo wangu na rafiki yangu. Kama mnavyojua, misiba hutufanya tuwe wamoja, tunyenyekee na mara nyingine hujenga hata urafiki uliokuwa na mashaka.”

Mwenyekiti Mstaafu wa chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Taifa, Freeman Mbowe akizungumza katika mazishi ya Mama wa Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe

Ameongeza kuwa licha ya tofauti zilizowahi kuwepo, ni muhimu jamii kujenga moyo wa msamaha na kuendelea na maisha.

“Ndugu yangu Sabaya pole kwa kuwa sijakuona siku nyingi, nilipokuja hapa nilikuta unaelezea kidogo katika maeneo fulani… sasa na mimi vilevile ni Graduate (mhitimu) na mimi nimepitia hivyo hivyo kwa taratibu tofauti, sasa ndugu zangu mnaweza mkajiweka kwenye nafasi yangu, ninachojaribu kukifikisha kwenu ni kuwatia moyo familia na kuwaambia ndugu zangu, waombolezaji wote, kuna maisha nje ya siasa.”

Mbowe pia amewataka viongozi waliopo madarakani kusimamia haki kwa manufaa ya Taifa.

“Taifa hili ni letu sote, unyenyekevu tunaouonyesha hapa leo tuishi nao siku zote, tunahitajiana, wale waliopo kwenye madaraka, kwenye nafasi za maamuzi, kwenye nafasi za uongozi wasimame katika misingi ya kuhakikisha haki inatendeka katika taifa ili kila mmoja katika taifa awe na sura ya tabasamu katika uso wake,” amesema Mbowe

Amesema: “Lakini Sabaya tumeshamsamehe kabisa watu Hai, maisha lazima yaendelee, kwa hiyo ukiniona ndugu yangu Sabaya hata nyumbani njoo kahawa nitakupa, sina kisasi, roho yangu ni nyeupe kama nilivyo siku zote kwa hiyo ndugu yangu Sabaya jisikie amani mimi nimeshakuombea msamaha kwa watu wa Hai siku nyingi sana.”

Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya akizungumza kwenye mazishi ya Mama wa Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe

Kwa upande wake, Lengai Ole Sabaya amesema changamoto alizopitia zimemfanya kubadilika na kuwa mtu mpya.

“Nilikuwa DC wa Hai kwa miaka kadhaa ( miaka miwili kasoro ) kabla ya kufanya ukorofi kidogo, Mungu akaenda kuutafuta uso wangu gerezani na toka wakati huo ninyi mnaona tembea yangu imebadilika, utagundua ongea yangu sasa ni ya heshima, mtaona kwamba Mungu amenibadilisha nimekuwa mtu bora, yaani amenifanya kuwa chuma chake,” amesema Sabaya.

Ameongeza kuwa uhusiano wake na Mbunge Saashisha Mafuwe ni wa karibu, akisisitiza kuwa anajitambua zaidi baada ya kupitia changamoto hizo.

Amesema, “Nimekuja kwenye msiba wa mama ninayemfahamu, wewe (Saashisha) ukifiwa na mama ni mimi nimefiwa na mama, nimekuja kukwambia tu kwamba wakati ule nikiwa gerezani ulipigana na mimi kufa kupona, kule ni nusu ya kuzimu, ukipitishwa pale hujabadilika basi wewe ni wa kuondoka na kufa, ndio maana mnaona hata sasa hivi, mabadiliko yangu yamekuwa makubwa sana.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *