
Njombe. Jeshi la polisi mkoani Njombe limesema kuwa limeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya mkoa huo na kuwaonya watakaofanya vitendo vya uhalifu kuelekea sherehe za Mei Mosi ambazo kitaifa zinafanyika mkoani Njombe.
Hayo yamesemwa leo Aprili 24, 2026, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani hapa.
Amesema mkoa huo umeteuliwa kuandaa sherehe za Mei Mosi kitaifa na kunatarajiwa kuwa na ugeni mkubwa hivyo wananchi wa Njombe wageuze kuwa fursa na siyo vitendo ambavyo siyo vya kiungwana.
Amesema wananchi wachukue tahadhari ya nyumba zao pamoja na kuwalinda watoto wao wakati wa kwenda shuleni na maeneo mengine kwakuwa idadi ya magari imeongezeka mkoani humo.
Amesema jeshi hilo limeimarisha doria katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo wakiwemo askari wa usalama barabarani ili kuhakikisha madereva mkoani humo wanafuata sheria za usalama barabarani.
“Nitoe wito kwa watu ambao wanafanya vitendo vya uhalifu kwamba Njombe tupo macho hivi sasa tunafanya doria masaa ishirini na nne kuhakikisha huu mkoa unakuwa salama” amesema Banga.
Amesema kwa wale madereva ambao hawafuati sheria za usalama barabarani hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ili kuhakikisha sherehe za sikukuu za wafanyakazi zinapita salama.
Amesema wilaya zote za mkoa huo ulinzi umeimarishwa na kwamba wapo wageni ambao wamepanga kwenye nyumba za watu hivyo wawe waaminifu ili siku wanapoondoka wasije wakabeba mali za watu.
Amesema wageni wanaofika mkoani humo wajue kuwa kuna uchache wa nyumba lakini hiyo ni fursa kwa wananjombe kulingana na mkuu wa mkoa Anthony Mtaka anavyoutendea haki mkoa huo wategemee kuona matukio makubwa yakiendelea kufanyika ndani ya mkoa huo.
Baadhi ya wafanyabiashara mkoani Njombe wamesema ujio wa wageni mkoani humo kutoka na sherehe za Mei Mosi imekuwa fursa kwa baadhi ya wafanyabiashara hususani wamiliki wa nyumba za wageni lakini kwa upande wa wafanyabiashara wa vyakula ni tofauti.
Mfanyabiashara wa kuuza chipsi mkoani Njombe Johnson Cholobi amesema ujio wa wageni kwao sio fursa kwani wageni wengi wanakula kwenye hoteli kubwa hivyo wao wenye vibanda vya chipsi hawanufaiki na ugeni huo.
“Wageni wa kawaida wanaokuja kufanya biashara Njombe kwa sasa hawaingii kwakuwa huduma za kulala hakuna zimejaa hivyo tunakosa fursa ya kufanya biashara,” amesema Cholobi.
Ameshauri wakati mwingine wageni wanapokuja Serikali itengeneze mazingira ya wageni kuchangamana na wenyeji ili hata wafanyabiashara wakiwemo maofisa usafirishaji wapate fursa tofauti na sasa wageni wanatumia magari waliyokuja nayo.